Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto
Biteko amewataka walimu nchini kuwasilisha changamoto zao na Serikali ipo
tayari kuzipatia ufumbuzi na imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali za kuboresha
maslahi yao na pamoja mazingira bora ya kazi.
Dkt. Biteko ameyasema hayo Februari 26, 2025 mkoani Geita
wakati aliposhiriki katika ‘Samia Teacher’s Mobile Clinic - Geita’ inayolenga
kusikiliza na kutatua kero za walimu Mkoani Geita.
“ Walimu semeni shida zenu na wakati wote msijione duni,
oneni namna Serikali inavyoweza kutatua changamoto zenu. Nataka niwakumbushe
Watanzania kuwa ninyi ni nguzo ya taifa
letu, zoezi hili linamfanya mwalimu mwenyewe kukutana na watoa huduma
Serikalini ili kujua nini kitafanyika juu ya changamoto yake,” amesema Dkt.
Biteko.
Ameendelea kusema kuwa Serikali inayoongozwa na Mhe. Rais
Samia Suluhu Hassan itaendelea kutatua changamoto za walimu na kwa kuwa nchi
zote zilizoendelea zimewekeza katika elimu.
Ametaja jitihada mbalimbali zilizofanywa na Serikali katika
kipindi cha miaka minne kuwa Serikali imelipa malimbikizo ya mishahara ya
walimu wa shule za msingi na sekondari kwa walimu 5,061 yenye thamani ya jumla
ya shilingi 4,753,349,209.00.
Kwa upande wa madeni ya uhamisho mkoani Geita, Serikali
imelipa jumla ya shilingi 2,207,540,900.00 kwa walimu 1,024.
“ Serikali imeendelea kupandisha walimu madaraja kwa wakati
na mserereko kwa walimu waliocheleweshwa. Katika mwaka wa fedha 2023/24 jumla
ya walimu 10,839 walipandishwa kawaida na walimu 509 walipandishwa madaraja ya
mserereko baada ya kubainika kuwa wamecheleweshwa madaraja yao,” amesisitiza
Dkt. Biteko.
Amesema ukokotoaji wa gharama za mabadiliko ya gharama za
kuwabadilishia walimu hao madaraja ni shilingi
5,471,025,529.00 kwa walimu waliopanda kawaida. Aidha, zilitumika
shilingi 368,771,480.00 kwa walimu waliopanda kwa mserereko. Pia, jumla ya
walimu 876 wamebadilishiwa muundo wa utumishi wao katika kipindi cha miaka
minne baada ya kujiendeleza na kuwasilisha vyeti vyao kwa waajiri.
Akizungumzia madai ya walimu waliokwenda likizo, Dkt. Biteko
amesema katika kipindi cha miaka minne, Serikali imeweza kulipa jumla ya
shilingi 4,255,813,700.00 kwa walimu 11,783. Piq, imelipa shilingi 25,690,000.00
kwa walimu ikiwa ni gharama za matibabu pale ambapo bima ya afya haihusiki
katika matibabu au ikiwa ni gharama za posho ya mtumishi
pindi anapohudhuria matibabu katika hospitali za rufaa.
Aidha, Serikali imeendelea kujenga mazingira wezeshi kwa
ajili ya kujifunzia na kufundishia ambapo kwa kipindi cha mwaka 2021 hadi 2024
mkoa wa Geita umejengewa shule mpya 154, kati ya hizo za msingi ni 74 na za sekondari ni shule 80.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amewataka wakurugenzi na
wakuu wa wilaya kuanzisha kliniki ndogo za kusikiliza changamoto za walimu
katika maeneo yao.
“ Niwapongeze CWT kwa kufanya hivi na kutumia raslimali kwa
ajili ya kutetea maslahi ya walimu. Kifanyeni chama chenu kiwe imara,
kiwahudumie walimu na sisi Serikali hatutaacha kusikiliza chochote
kitakachotoka katika chama chenu,” amesema Dkt. Biteko.
Pamoja na hayo Dkt. Biteko amekitia moyo kikosi kazi cha
maafisa waandamizi kutoka Ofisi mbalimbali Serikalini wanaosikiliza na kutatua
kero za walimu kufanya kazi hiyo kwa bidii na hatimaye kupata matokeo chanya.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi,
Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi amekipongeza kikosi kazi
kwa kufanya kazi nzuri ya kutatua changamoto za walimu kwa kushirikiana na CWT.
“ Baada ya kazi kukamilika itaweka misingi kwa watumishi wa
umma kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia miongozo iliyopo,” amesema Mhe.
Katambi.
Katibu Mkuu wa Chama Cha Walimu Tanzania (CWT), Bw. Joseph
Misalaba amesema kuwa zoezi la kliniki hiyo ni matokeo ya kufanyika kwa ziara
mwaka 2024 mkoani Mwanza iliyohusisha maafisa utumishi ambayo ililenga kukutana
na walimu wenye chamgamoto sa kiutumishi na kuzitatua.
“ Walimu wengi wekitokeza na changamoto za kiutumishi na
idadi kubwa ya walimu waliojitokeza ambayo imetupatia tafsiri walimu wengi wana
changamoto za kiutumishi ambazo zingestahili kutatuliwa na waajiri wao katika
maeneo yao,” amesema Bw. Misalaba.
Ametaja baadhi ya changamoto hizo ni madai mengi ya
malimbikizo ya mishahara ambayo hayajaingizwa katika mfumo, uwepo wa walimu
waliomba kubadilishiwa miundo maombi ambayo hayajafanyiwa kazi kwa wakati.
Aidha, Kliniki hiyo inaratibiwa na Chama Cha Walimu Tanzania
kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Ofisi ya Rais
TAMISEMI, Wizara ya Fedha, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Tume
ya Utumishi wa Walimu – TSC.
Aidha, timu ya maafisa waandaizi kutoka katika Ofisi za Serikali imefanyakazi katika mikoa 20 hadi sasa.
0 Maoni