WAKATI masoko ya madini yakifikia 43, mchango wa masoko hayo
umeongezeka kutoka Shilingi Bilioni 8 mwaka 2018/ 2019 hadi Shilingi Bilioni
183 mwaka wa fedha uliomalizika wa 2023/2024.
Akizungumza katika mafunzo ya matumizi ya mashine maalum ya kupima madini
ya metali kwa njia ya MIONZI /X-RAY, kwa
maafisa masoko wa madini Mkurugenzi wa Ukaguzi na Biashara ya Madini, Venance
Kasiki amesema mbali na masoko hayo pia kuna vituo vya ununuzi wa madini 109.
Amesema, “Kwa kuzingatia asilimia kubwa ya mapato yetu
katika masoko yanatokana na madini ya dhahabu, na ili tupate maduhuli lazima
tutumie mashine za XRF kupima asilimia (purity) ya madini yanayouzwa. Majibu
yanayotokana na XRF yanatumika kukokotoa mrabaha na ada ya ukaguzi.”
Kwa upande wa Meneja wa Biashara ya Madini Sundi Malomo
akizungumza amesema kuwa tangu Serikali kupitia Tume ya Madini kuanzisha masoko
ya madini Mei, 2019 kama mkakati wa kuimarisha biashara ya madini nchini,
masoko hayo yamekuwa na mchango mkubwa wa kuongeza mapato ikiwemo kutoa ajira.
“Ili kuimarisha ukusanyaji wa maduhuli kama mnavyofahamu
Sekta ya Madini inatakiwa ichangie asilimia 10 katika Pato la Taifa kwa mwaka
wa Fedha 2024/2025, Tume ya Madini imepewa lengo la kukusanya Shilingi Trilioni
1, hivyo tumewapa mafunzo maafisa masoko na kuwakumbusha majukumu ya Idara-
sehemu ya biashara,”amesema Sundi na kuongeza.
“ Katika mafunzo haya tumeweza kuainisha changamoto
tulizonazo na kuweza kuonyesha mchango wa masoko kuanzia mwaka 2018/2019 ambapo
mchango wa masoko ulikuwa ni Shilingi Bilioni 8, mchango huo umeongezeka kwa
kiasi kikubwa mwaka hadi mwaka, mwaka wa
fedha 2023/2024 masoko haya yameweza kuchangia takribani Shilingi Bilioni
183,”amesema Sundi.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa Ukaguzi na Biashara ya
Madini, Venance Kasiki amesema ili kuhakikisha mashine za XRF zinatumika vizuri
na lengo kusudiwa linapatikana, wameamua kufanya mafunzo kwa watumiaji wa vifaa
hivyo waliopo kwenye masoko ya madini mikoa yote ya Tanzania Bara.
Aidha, amesema wamemualika mtaalam kutoka Kampuni ya Thermo
Fisher Scientific ya Afrika Kusini ambao ndio watengenezaji wa mashine hizo, Mirko
Steinhage kutoa elimu zaidi juu ya matumizi sahihi ya XRF.
Kwa upande wake Kaimu Meneja Ukaguzi Madini na Huduma za
Maabara, Mhandisi Mvunilwa Mwarabu amesema mafunzo hayo ni fursa njema kwa kuwa
mashine za XRF na Mizani ndio vinasaidia katika ukusanyaji wa maduhuli ya
Serikali hivyo ni muhimu zikatumika kwa ubora ili kubaini kiasi sahihi cha
madini na Serikali ipate mapato yake sahihi.
Amesema, ni imani yake kuwa baada ya mafunzo hayo vifaa vitatumika kwa usahihi, tija na kasi ya ukusanyaji maduhuli itaongezeka.
0 Maoni