Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kupitia
Pori la AKiba Pande imepanga kuongeza idadi ya wanyamapori takribani 100 kwa
ajili ya kuongeza mazao mbalimbali ya utalii katika hifadhi hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 4, 2025,
Afisa Utalii wa Pori la Akiba Pande, Mustapha Buyogera amesema hadi sasa
hifadhi hiyo ina aina mbalimbali za wanyamapori kama vile simba, duma, mamba,
pundamilia, nyumbu, pofu, swala pala, swala granti, mbuni, chatu, na White
Colobus monkey.
“Hadi sasa Hifadhi ya Pande ina wanyamapori takribani 60
lakini tunakwenda kuongeza wanyama takribani 100 katika hifadhi hii ili
kuhakikisha wageni wakifika hapa wanafurahia vivutio vilivyopo ndani ya
hifadhi, tunataka kuifanya Pande kuwa kitovu cha utalii katika jiji la Dar es
Salaam,” amesema Buyogera.
Sambamba na uongezwaji wa spishi mbalimbali za wanyamapori,
Buyogera amesema kuwa TAWA imeboresha miundombinu mbalimbali ndani ya hifadhi
ili kuhakikisha mtalii akitembelea hifadhi hiyo anapata huduma zote muhimu ikiwemo
malazi na sehemu za kupumzika.
Miongoni mwa miundombinu iliyoboreshwa ni pamoja na ujenzi
wa barabara ya kilometa 10.5, geti la kuingilia hifadhini, sehemu ya kupumzikia
wageni (Picnic Site), kambi za Watalii (Camp Sites), njia za utalii (Tourism trail)
pamoja na vyoo vya watalii.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha
Mapinduzi, Tawi la Mabwepande James Mbugi alipata wasaa wakutembelea hifadhi ya
Pande na amesema kuwa Serikali chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe.Dkt Samia Suluhu Hassan inafanya makubwa katika sekta ya utalii
na matokeo yanaonekana dhahiri.
“Ilikuwa ni nadra eneo kama Mabwepande kupata hifadhi yenye
viwango kama hii kwa sisi tuliozunguka tumeona wanyama wa aina mbalimbali, kuna
uwekezaji mkubwa kwelikweli ambao umefanyika hapa,” amesema James.
Aidha, ndugu James alitoa rai kwa viongozi vijana na wananchi kwa ujumla kutembelea hifadhi ya Pande kuja kujionea vivutio vya utalii vilivyopo jijini Dar es Salaam.
0 Maoni