Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) amezielekeza halmashauri zote nchini kuchukua jukumu la kulinda wananchi dhidi ya wanyamapori wakali na waharibifu kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii na taasisi zake.
Ameyasema hayo leo Februari 4, 2025 Bungeni jijini Dodoma
alipokuwa akitoa ufafanuzi kuhusu swali la Mhe. Mhandisi Ezra John Chiwelesa
aliyetaka kujua Serikali ina mpango gani
wa kuondoa adha ya uvamizi wa tembo katika Kijiji cha Nyabugombe Kata ya
Nyakahura – Biharamulo.
“Katika bajeti za halmashauri asilimia 10 za bajeti za
halmashauri , mapato ya ndani na kuna maeneo Wizara ya Maliasili na Utalii
inarudisha fedha za Wildlife Management Areas asilimia 25, fedha hizi
zinatakiwa zitumike kwa shughuli rafiki za uhifadhi kulinda wananchi
wasiumizwe” amesisitiza Mhe. Chana.
Amesema kuwa ajenda ya kulinda wananchi dhidi ya changamoto
mbalimbali ikiwemo za wanyamapori wakali na waharibifu ni ajenda ya halmashauri
husika na kusisitiza kwamba halmashauri zina uwezo wa kununua ndege nyuki
“drones”, kusomesha vijana kozi za uhifadhi ili wawe Askari wa Vijiji wajue
namna ya kulinda wananchi.
Awali akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Maliasili na
Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula (Mb) alifafanua kuwa Serikali inaendelea
kutekeleza mikakati mbalimbali ya kukabiliana na adha ya wanyamapori wakali na
waharibifu wakiwemo tembo katika maeneo yanayopakana na Hifadhi ya Taifa Burigi
– Chato.
“Mikakati inayotekelezwa ni pamoja na: kuendelea
kushirikiana na Wananchi kudhibiti tembo kwa wakati ambapo jumla ya Askari sita
(6) wa uhifadhi kwa kushirikiana na mgambo sita (6) waliopewa mafunzo kuhusu
tabia za wanyamapori wanatumika kufukuza tembo kupitia kituo cha Nyungwe
kilichopo Kijiji cha Nyabugombe, Kata ya Nyakahura,” alisema Mhe. Kitandula.
Kijiji cha Nyabugombe kilichopo katika Kata ya Nyakahura, ni miongoni mwa vijiji 38 vinavyopakana na Hifadhi ya Taifa Burigi-Chato. Kwa kipindi cha miezi sita Julai – Disemba, 2024 Jumla ya matukio 16 ya tembo yaliripotiwa na kudhibitiwa katika kijiji cha Nyabugombe kilichopo Kata ya Nyakahura, Wilaya ya Biharamulo.
0 Maoni