Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu
Hassan, ametoa wito kwa wanawake waliobahatika kupata fursa ya elimu na kuwa
viongozi kwenye maeneo mbalimbali nchini kuhakikisha kuwa wanafanyakazi kwa
bidii, weledi na uadilifu ili kuongeza imani kwa jamii kuhusu umuhimu wa elimu
kwa mtoto wakike.
Dkt. Samia ametoa wito huo leo kwenye maadhimishio ya miaka
10 tangu kuanza kwa Mafunzo ya Uongozi kwa Wanawake Tanzania (Female Future
Program) yaliyoambatana na Mahafali ya Wahitimu wa Awamu ya 10 ya mafunzo hayo
na Mkutano wa 7 wa Uongozi, yaliyofanyika kwenye ukumbi wa The Super Dome Masaki,
Dar es Salaam.
Aidha, Rais Samia amewataka wahitimu hao kuwa chachu ya
maendeleo katika jamii na kutumia elimu na stadi za uongozi walizopata
kunufaisha jamii.
Vilevile, Rais Dkt. Samia ametoa rai kwa wanawake
kudhihirisha ushupavu wa uongozi kwenye mashirika na taasisi mbalimbali wanayofanyiakazi
na kuwataka kuwa wabunifu na kwenye kazi zao na kuwa waaminifu katika kulipa
kodi ili kuwezesha na utekelezaji wa miradi mbalimbali inayogusa maisha ya
wananchi.
Kwa upande wa ustawi wa jamii, Rais Dkt. Samia amewausia
wanawake kuwa pamoja na elimu na nafasi za uongozi walizonazo, wasiache wajibu
wao wa kijamii wa malezi na makuzi ya watoto ili kuwaepusha kujiingiza kwenye
mienendo isiyofaa.
Kuhusu uchaguzi mkuu ujao, Rais Dkt. Samia amewahamasisha wanawake wenye sifa na uwezo kujiandikisha kupiga kura na kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi zitakazowaniwa katika uchaguzi huo.


0 Maoni