Askari wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania- TAWA wamefanikiwa kumvuna fisi I mmoja Februari 20, 2025 na kufanya Idadi ya fisi waliovunwa kufikia 17 tangu Oparesheni Maalumu ya kuwadhibiti wanyamapori ianze tarehe 25 Januari, 2025 Mkoani Simiyu.
Fisi huyo aliyeuawa amekutwa akiwa na chata pamoja na kuandikwa
jina la mtu upande wa paja lake la kushoto, huku akiwa na shanga shingoni.
Kufuatia tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Anna Gidarya
amewataka wananchi wote wilayani humo wanaomiliki nyara za Serikali kinyume cha
sheria kuzisalimisha haraka kwa wahusika wa uhifadhi, kabla ya hatua kali
hazijachukuliwa dhidi yao.
Kumekuwepo na matukio ya fisi kushambulia watoto kuanzia
majira ya saa moja usiku katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Itilima.
Takwimu zilizotolewa wilayani Itilima zinaonyesha kuwa kuanzia mwaka 2024 hadi sasa watu nane wamefariki dunia baada ya kushambuliwa na fisi na wengine 17 wamejeruhiwa, huku fisi 16 wakiuawa katika kipindi hicho.


0 Maoni