Mwenyekiti wa
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) Mhe. Augustine
Vuma Holle (Mb) amesema Kamati yake imeridhishwa na utekelezaji wa miradi ya
miundombinu ya utalii inayofanywa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori
Tanzania - TAWA katika Hifadhi ya eneo la Makuyuni Wildlife Park iliyopo wilaya
ya Monduli Mkoani Arusha.
Mhe.
Augustine ameyasema hayo leo Februari 9, 2025 wakati Kamati yake ilipotembelea
hifadhi hiyo kwa lengo la kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na TAWA katika
eneo hilo.
"Kamati
imefurahishwa na namna ambavyo miradi inaendelea, ikumbukwe kwamba hili eneo
mara ya kwanza lilikuwa chini ya mwekezaji Kwa muda mrefu sana, baada ya
Serikali kuona kwamba hakuna tija eneo hili kuendelea kukaa Kwa mwekezaji,
ikalichukua eneo hili na kukabidhiwa msajili wa hazina lakini baadae msajili wa
hazina aliwakabidhi TAWA ili waweze kuliendeleza" amesema Mhe. Augustine.
"Kamati
imeona na imeshuhudia pasipo na shaka kwamba uwekezaji unafanyika na unafanyika
kwa utaratibu ambao unafaa na kwakweli tija ya uwekezaji ipo kwasababu mapato
yameanza kuongezeka na tunaamini yataendelea kuongezeka. Kwahiyo TAWA
wataendelea kufanya uwekezaji hapa kwasababu tumeona kwamba imeanza kulipa,"
ameongeza.
Aidha,
Mwenyekiti huyo wa Kamati ya PIC ametoa wito Kwa watanzania wote na wakazi wa
mkoa wa Arusha na mikoa jirani na Arusha kutembelea eneo hilo ili kujionea
vivutio mbalimbali vya utalii.
"Nitoe
rai kwa watanzania wote, kwakweli Makuyuni Wildlife Park ni sehemu nzuri sana
ya kuja kutembelea, yaani ukija humu ndani hutamani kutoka, kuna wanyamapori wa
kila aina kuna twiga, tumeona simba, tembo, swala kwakweli ni kituo cha kuvutia
watalii," amesema.
Kwa upande
wake Naibu Waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii Mhe. Dunstan Kitandula amesema tangu TAWA ikabidhiwe eneo hilo Idadi
ya wanyamapori imeongezeka Kwa kiasi kikubwa
na pia fedha zinazotokana na uwekezaji uliofanyika zimeongezeka ambapo
amesema kuwa Kwa kipindi cha Mwaka mmoja TAWA imeweza kukusanya zaidi ya
shillingi Millioni 200 jambo ambalo linathibitisha kuwa ni mwanzo mzuri na
wenye kuleta matumaini makubwa.
Sambamba na
hilo Mhe. Kitandula amesema kutokana na uwekezaji unaondelea kufanywa na TAWA
Wizara inatarajia TAWA kuongeza mapato ya zaidi ya Billioni 20 Kwa mwaka jambo
ambalo Taasisi hiyo imeihakikishia Wizara kuwa inawezakana.
Naye
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TAWA Mej. Jen. (Mstaafu) Hamis R. Semfuko
amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan Kwa kuipatia TAWA eneo la Makuyuni Wildlife Park ili iweze kulitumia Kwa
ajili ya shughuli za utalii.
Vilevile
Semfuko amesema TAWA imejijengea utamaduni wa kuwa na matumizi sahihi ya fedha
hasa fedha zinazotolewa na Serikali Kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
"Hii
ndio tabia yetu TAWA kuhakikisha ya kwamba kila senti ambayo Mheshimiwa Rais
anaitoa inatumika kama ilivyopangwa na Kwa ubunifu mkubwa"
amesisitiza Semfuko.
Na. Beatus
Maganja - Arusha
0 Maoni