Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu
Hassan, amesema kuwa kukamilika kwa ujenzi wa kiwango cha lami barabara
inayounganisha Tanga, Pangani, Saadani na Bagamoyo pamoja na Daraja la Mto
Pangani lenye urefu wa mita 525 zitasaidia kuifungua Tanga Kiutalii na
kiuchumi.
Rais Samia ameyasema hayo leo, Februari 26, 2025 wakati wa
uwekaji wa jiwe la msingi katika ujenzi wa
barabara na Daraja la Mto Pangani ikiwa ni sehemu ya muendelezo wa ziara
yake mkoani Tanga. Vilevile, alisisitiza kuwa miundombinu hiyo mipya
itarahisisha maeneo mengi ya utalii kufikika kiurahisi.
Rais Samia alieza “Barabara hii tunayoiunganisha inaenda
kuifungua Tanga kiutalii na kibiashara. Maeneo mbalimbali ya kiutalii ambayo
hayafikiki, itakuwa ni rahisi kumtoa mtalii Hifadhi ya Taifa Saadani na kwenda
kutalii maeneo mengine ndani ya Mkoa wa Tanga.”
Naye, Mbuge wa jimbo la Pangani Mhe. Jumaa Aweso alimshukuru
Rais Samia kwa kutekeleza mradi mkubwa wa barabara na Daraja ambayo yatachochea
maendeleo ya kiuchumi ndani ya Wilaya ya Pangani.
“Barabara hii ya Tanga, Pangani, Saadani na Bagamoyo
itachochea uwekezaji ukizingatia Pangani tuna Hifadhi ya Taifa Saadani, Hifadhi
pekee inayopakana na Bahari ya Hindi. Tukipata “Fast Boat” shida ya
usafirishaji itaisha na watalii watapita kutoka Zanzibar kuja kutembelea
Saadani” alisema Mhe. Awesu.
Hifadhi ya Taifa Saadani ni moja kati ya Hifadhi za Taifa 21
Tanzania yenye upekee wake wa mandhari ya nyika kukutana na bahari katika eneo
moja ambapo ni kivutio kikubwa cha utalii kwa ukanda wa pwani.
Ziara hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali akiwemo Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana (Mb) pamoja na wakuu wa taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii akiwemo Kamishna wa Uhifadhi TANAPA.
Na. Philipo Hassan - Tanga
0 Maoni