WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amezitaka taasisi za dini
nchini kuendelea kuwahamasisha waumini wake kudumisha amani na kushiriki katika
shughuli za maendeleo.
Ameyasema hayo leo (Jumanne, Januari 14, 2025)
alipokutana na viongozi wa Kitaifa wa Jumuiya ya Kiislam ya Ahmadiyya ofisi
ndogo ya Waziri Mkuu Oysterbay jijini Dar es Salaam. Viongozi hao wapya wa
jumuiya hiyo walikwenda kwa ajili ya kijitambulisha.
“…Fanyeni kazi kwa uhuru na wala msiwe na mashaka.
Wahamasisheni Watanzania washiriki katika shughuli za kimaendeleo.” Pia
amewashauri viongozi hao wabuni miradi ya kiuchumi kwani Tanzania kuna fursa
nyingi za kimaendeleo.”
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa ameipongeza jumuiya hiyo
kwa uwekezaji iliofanyika katika sekta mbalimbali zikiwemo afya na elimu ambapo
ameahidi kuwa Serikali itaendelea kuwapa ushirikiano katika jitihada zao hizo.
Amesema Serikali kwa upande wake inathamini na kutambua
mchango mkubwa unaofanywa na taasisi mbalimbali za kidini nchini ikiwemo
Jumuiya ya Kiislam ya Ahmadiyya, hivyo amewahakikishia ushirikiano katika
utekelezaji wa majukumu yao.
Kwa upande wake, Amiri na Mbashiri Mkuu wa Jumuiya ya
Kiislamu ya Ahmadiyya, Sheikh, Khawaja Muzaffar Ahmad ameipongeza Serikali ya
Tanzania kwa kazi nzuri inayofanywa katika kuwahudumia Watanzania. “Nimeishi
Tanzania kwa zaidi ya miaka 20, ni nchi nzuri hongereni kwa kazi nzuri
mnazozifanya.”
Naye, Naibu Amiri, Sheikh Abdulrahman Mohammed Ame
ametumia fursa hiyo kuishukuru Serikali kwa kuwajali wananchi wake na
amemuahidi Waziri Mkuu kwamba taasisi yao iko tayari kushirikiana na Serikali
katika masuala mbalimbali yakiwemo ya uwekezaji.
0 Maoni