Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali
za Mitaa Mhe. Mohamed Mchengerwa amewataka watumishi wa umma wanaohudumu chini
ya ofisi yake kutojiusisha na shughuli za siasa kama ambavyo Sheria, Kanuni na
Taratibu za utumishi wa umma zinavyoelekeza.
Waziri Mchengerwa ametoa maelekezo hayo jana, wakati akijibu
hoja za baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa inayoendelea na vikao vyake vya kawaida jijini Dodoma chini
ya Mwenyekiti wake Mhe. Justine Nyamoga.
“Kwa mujibu wa Kanuni F.21 (b) ya Kanuni za Kudumu katika
Utumishi wa Umma toleo la Mwaka 2009 mtumishi wa umma harusiwi kujihusisha na
shughuli za kisiasa wakati akiendelea kutekeleza majukumu yake ya kiutumishi,
hivyo ofisi yangu haitosita kuwachukulia hatua za kinidhamu watumishi wote
wanaokiuka kanuni hiyo,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.
Mhe. Mchengerwa amewaelezea wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kuwa, Ofisi yake haiungi mkono
watumishi wanaoacha kutekeleza majukumu yao ya msingi na badala yake
wanajishughulisha na masuala ya kisiasa ambayo yanaathiri utoaji wa huduma kwa
wananchi.
Mhe. Mchengerwa ameongeza kuwa, uwepo wa baadhi ya watumishi
wanaotumia rasilimali za Serikali kufanya shughuli zao za kisiasa ni jambo
ambalo hawezi kulifumbia macho na kueleza kuwa tayari ameshatoa maelekezo kwa
Katibu Mkuu OR-TAMISEMI kufuatilia kwa ukaribu madai hayo ili hatua stahiki
zichukuliwe.
“Taratibu ziko wazi kama kuna mtumishi anahitaji kuingia kwenye siasa anapaswa kuzingatia taratibu za kiutumishi ikiwepo kumfahamisha mwajiri wake na kwa baadhi ya nyadhifa mtumishi anapaswa kujiudhuru ili aingie moja kwa moja kwenye siasa, hivyo ninashauri watumishi wa umma kuzingatia Kanuni, Sheria, Taratibu na Miongozo ya Utumishi wa Umma iliyopo,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.

0 Maoni