Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Mhandisi Chagu Ng'homa
amewataka wadau wa ununuzi nchini kuutumia ipasavyo mfumo mpya wa Kielektroniki
wa Manunuzi ya Umma (NeST), ili kusaidia kupata wazabuni zenye gharama zinazolingana
na thamani ya fedha zinazolipwa.
Ng’homa ametoa wito huo leo tarehe 20 januari, 2025 kwa
niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza wakati
akifungua mafunzo yaliyofanyika Rock City Mall- Mwanza ya mfumo wa Usimamizi na
Ununuzi wa Umma Kielektroniki yaliyowakufanisha washiriki kutoka taasisi
mbalimbali nchini.
Amesema, washiriki wanapaswa kuwa wazalendo kwenye kazi
zao kwa kuzingatia kuwa wanatakiwa kulinda rasilimali fedha za nchi wakati wa
ununuzi kwa kuwashindanisha wazabuni kwa mujibu wa sheria.
"Mfumo huu umeletwa mahsusi ili kusaidia kuongeza
wigo wa ushiriki wa wazabuni, kukidhi mahitaji na matarajio ya watumiaji pamoja
na kurahisisha mchakato wauombaji zabuni hivyo nendeni mkazingatie hayo ili
kulisaidia taifa," amesema Chagu.
Aidha, ametoa wito kwa Mamlaka ya Ununuzi wa Umma (PPRA)
kuendelea kuboresha mfumo wa NeST ili kuweka mazingira rafiki kwa wazabuni na kutoa
mafunzo kwa taasisi za ununuzi ili kufikia malengo yalivyokusudiwa.
Vilevile, ametoa pongezi kwa mamlaka hiyo kwa jinsi
wanavyoendelea kuboresha mfumo huo ambao Mhe. Rais Samia mwenyewe aliuzindua
mahususi kwa ajili ya wadau kufuatilia mchakato kwa uwazo na kuona thamani ya
fedha.
Akiongea kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa PPRA Robert
Kalunde amesema wameandaa mafunzo hayo ya siku 5 yanayowakutanisha washiriki
zaidi ya 230 kutoka taasisi mbalimbali nchini ili waujue vizuri mfumo huo na
kufikia malengo kwenye ununuzi.
0 Maoni