Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Andrea
Mathew (Mb) ametembelea na kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa maji
Dar es salaam ya Kusini maarufu kama Bangulo na kuridhishwa na kazi kubwa
iliyofanyika hadi sasa ya kufikisha mradi asilimia 97 ya utekelezaji.
Mhandisi Kundo amesema maeneo yaliyokuwa na
changamoto ya huduma ya maji kwasasa inakwenda kutibiwa na mradi huo wa maji
Bangulo na wananchi wategemee huduma bora ya majisafi.
"Niseme sasa muarobaini wa huduma ya
majisafi umepatikana katika maeneo ya Kinyerezi, Ukonga, Kitunda, Kibamba na
Mwanagati maeneo haya yaliyokuwa na changamoto ya majisafi sasa yanakwenda
kupata huduma ya kutosheleza," amesema Mhandisi Kundo.
Mhe Kundo amesema kazi kubwa inafanyika chini
ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuwafikishia wananchi huduma ya majisafi na
zote hizi ni jitihada za Mh. Rais wa awamu ya sita, Daktari Samia Suluhu Hassan
kumtua mama ndoo ya maji kichwani pamoja na kutekeleza ilani ya Chama Cha
Mapinduzi.
Mwakilishi wa Mbunge wa Ukonga Mheshimiwa
Jerry Silaa, ndugu Ayubu Mwaikotobwa ameeleza fedha hizi za utekelezaji wa
mradi wa maji Bangulo ni ishara kubwa ya upendo wa Mh.Rais kwa wananchi wa
Ukonga na meneo jirani yatakayonufaika na mradi na sasa wananchi wa maeneo hayo wanaimani kubwa
ya kupata huduma ya majisafi na salama yakutosheleza.
Mradi wa Maji Bangulo unaogharimu kiasi cha
shilingi Bilioni 36.8 utahudumia wakazi zaidi ya 450,000 huku ukijumuisha ujenzi
wa tenki kubwa la kuhifadhi maji lita Milioni 9 na ulazaji wa mtandao wa bomba
wenye Kilomita 108 na unategemea kukamilika
Januari 30, 2025.
0 Maoni