Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro (NCAA) imezindua Kampeni ya kuhamasisha utalii wa ndani katika mapango ya amboni Tanga kuelekea sikukuu ya wapendanao inayoadhimishwa kila mwaka tarehe 14 Februari.
Kampeni hiyo iliyozinduliwa na Mkuu wa Wilaya ya Tanga Mhe.
Japhari Kubecha leo tarehe 26/01/2025, inaenda kwa kauli mbiu isemayo
"Diko la Amboni: Furaha ya Asili,Utajiri wa Urithi," ambapo pamoja na kuhamasisha utalii wa ndani
kampeni hiyo inalenga kukuza uchumi wa wajasiriamali wadogo katika mkoa wa
Tanga.
Akizunguza katika uzinduzi huo, Mhe. Kubecha aliipongeza
uongozi wa NCAA kwa juhudi za kuhamasisha utalii wa ndani katika mapango hayo
na kutoa rai kwa wananchi ndani na nje ya Mkoa wa Tanga kujenga utamaduni wa
kutembelea vivutio vilivyopo ndani ya nchi.
“tunatambua juhudi za pekee zinazofanywa na Mamlaka ya
Hifadhi ya Ngorongoro kuhakikisha kuwa utalii mambo kale na urithi wa utamaduni
unaendelea kuwa kivutio bora cha watalii nchini, kutokana na hili naomba nitoe
rai kwa wananchi wote ndani na nje ya mkoa wa Tanga kuhakikisha kuwa siku ya
tarehe 14, Februari tunakutana hapa Amboni,”alisema Mhe. Kubecha.
Kwa upande wake Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi,
NCAA anayesimamia huduma za utalii na masoko, Mariam Kobelo alisema kwamba
kuelekea siku hiyo NCAA itatoa nafasi kwa wakazi wa Tanga kushiriki kwenye
shughuli mbalimbali zitakazo fanyika hapo ili kuendelea kutoa hamasa na kuongeza uwelewa wa shughuli mbalimbali za
Uhifadhi zinazofanywa na Mamlaka hiyo.
“Shughuli hii ambayo tunaenda kuifanya msimu huu wa sikukuu
za wapendanao itahusisha mashindano ya Upishi wa vyakula vya asili, ambayo
yatafanyikia hapa amboni pamoja na kutembea ndani ya mapango na kupatiwa elimu
juu ya kivutio hiki cha kipekee kilichopo katika nchi yetu,” Alisema Mariam.
Aidha, Kobelo alieleza kuwa ili kuhakikisha siku hiyo
itakuwa nzuri na kuwezesha watanzania wengi kushiriki, Mamlaka imeshirikiana na
Kampuni ya Utalii ya Smiles Safaris
ambayo itatoa huduma za kuwaleta watalii amboni kutoka mikoa ya Dar es
salaam, Arusha, Kilimanjaro na Tanga ambapo gharama za ushiriki kwa kila Mkoa
zitatolewa na gharama hizo zitahusisha
Chakula, Malazi siku moja, viingilio pamoja na picha.
Mapango ya Amboni Tanga yanayosimamiwa na Mamlaka ya Hifadhi
ya Ngorongoro (NCAA) tangu mwaka 2019 na yapo umbali wa Km 9 tu kutoka katikati
ya Jiji la Tanga.
Mapango hayo yamefanyiwa maboresho mbalimbali ikiwemo ufungaji wa taa maalum kuwezesha mgeni kuona vivutio vilivyopo ndani ya Mapango sambamba na kuboresha njia za mapito katika eneo la ndani ya mapango hayo ambapo kwa sasa eneo hilo linapokea wageni zaidi ya 30,000 kwa mwaka.
Na. Philomena Mbirika - Tanga



0 Maoni