Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.
Dunstan Kitandula, amefanya ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo
inayotekelezwa chini ya Mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza
Utalii Kusini mwa Tanzania REGROW katika Hifadhi ya Taifa ya Mikumi.
Katika ziara hiyo aliyoifanya jana, Mhe.
Kitandula amekagua maendeleo ya miradi mbalimbali ya miundombinu, ikiwemo
ujenzi wa Kiwanja cha Kisasa cha Ndege, majengo ya kupokelea wageni, mageti
mawili ya kisasa, na nyumba za kisasa za kupumzikia wageni.
Mhe. Kitandula amewataka wasimamizi wa mradi
huo kutunza miundombinu ya kisasa inayojengwa, akisisitiza kuwa kukamilika kwa
miradi hiyo kutakuwa na manufaa makubwa kwa jamii na taifa kwa ujumla, huku
akisisitiza kuwa miradi hiyo itachochea ukuaji wa sekta ya utalii, kuboresha
huduma kwa wageni, na kuongeza idadi ya watalii katika hifadhi ya Taifa Mikumi,
jambo litakaloongeza mapato ya utalii na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika
maeneo ya jirani.
“Miundombinu hii ya kisasa ni muhimu katika
kufungua fursa za kiuchumi na kijamii, hususan kwa jamii zinazozunguka Hifadhi
ya Taifa Mikumi, tunahitaji kuhakikisha kwamba miradi hii inakamilika kwa
wakati ili wananchi waanze kunufaika na fursa zinazotokana na mradi huu,”
alisema Mhe. Kitandula.
Mradi wa REGROW, unaotekelezwa na Serikali ya
Tanzania, unalenga kuboresha miundombinu ya utalii, kuimarisha usimamizi wa
maliasili, na kuvutia uwekezaji katika sekta ya utalii. Kupitia mradi huo,
maeneo muhimu ya Hifadhi ya Mikumi yameboreshwa, yakiwemo miundombinu ya barabara,
vituo vya taarifa, na huduma bora za wageni. Mhe. Kitandula alisisitiza umuhimu
wa miradi hii katika kuimarisha sekta ya utalii, huku akiwataka wasimamizi
kuunga mkono jitihada za Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuisimamia vyema
na kuitunza miundombinu hiyo.
Naye, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa
Uhifadhi Kanda ya Mashariki John Nyamhanga, alieleza jinsi mradi wa REGROW
ulivyobadilisha muonekano wa Hifadhi ya Taifa Mikumi, huku akikazia namna
uboreshaji wa miundombinu hiyo utaongeza mazao ya utalii, hivyo kuhamasisha
ongezeko la idadi ya watalii na kukuza pato la Taifa.
Mradi wa REGROW katika hifadhi ya Taifa
Mikumi ni ushahidi wa dhamira ya Serikali ya Tanzania katika kutunza na
kuendeleza rasilimali za asili za nchi kwa ajili ya manufaa ya wananchi na
ustawi wa taifa.
Zainab Ally – Mikumi
0 Maoni