Serikali imeziagiza mamlaka na taasisi zinazosimamia na
kutumia kituo cha mafunzo ya Jeshi la Uhifadhi (JU) kilichopo Mlele mkoani
Katavi kufanyia kazi changamoto mbalimbali zinazokikabili kituo hicho.
Maelekezo hayo yametolewa na Naibu waziri wa Maliasili na
Utalii Mhe. Dunstan Kitandula (Mb) wakati akifunga mafunzo ya watumishi wa
taasisi za uhifadhi zinazotoa mafunzo ya Jeshi la Uhifadhi wa wanyamapori na
misitu yaliyofanyika kwa miezi mitatu
kwa lengo la kuwabadilisha watumishi waliojiunga na taasisi hizo hivi
karibuni kutoka katika mfumo wa kiraia kwenda mfumo wa kijeshi.
Mhe. Kitandula amesisitiza kuwa ni muhimu taasisi hizo
kuboresha miundombinu inayoklabili kituo hicho ikiwemo huduma za afya,
barabara, maeneo ya kujifunzia,vifaa pamoja na kuhakikisha kituo hicho
kinatumia nishati safi ya kupikia.
Katika risala yao wahitimu walimweleza mhe naibu waziri uwepo wa changamoto hizo ambapo
walisema kwamba ikiwa maboresho hayo
yatafanyika yataongeza tija na
ufanisi wa kujifunza kwa wanafunzi na wakufunzi kutumia muda wao vizuri wa
mafunzo.
Mheshimiwa Kitandula amewapongeza wahitimu wote na kuwataka
kutumia mafunzo hayo katika kuhakikisha kuwa wanalinda rasilimali za umma kwa
uadilifu,uzalendo,uaminifu na kufuata sheria na taratibu zote za serikali.
Akizungumza kwa niaba ya makamishna wa Uhifadhi zilizoko
chini ya wizara ya maliasili na Utalii, Kamishna wa Mamlaka ya Hifadhi ya
Ngorongoro Dr. Elirehema Doriye amesema maelekezo yote yaliyotolewa na serikali
yatafanyiwa kazi kwa kuunganisha nguvu ya taasisi zinazotumia kituo hizo ambazo
ni TANAPA,TFS, NCAA na TAWA.
Mratibu wa mafunzo hayo kutoka wizara ya Maliasili na Utalii Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi, Fidelis Kapalata ameeleza kuwa jumla ya wanafunzi 231 wamehitimu mafunzo ya mabadiliko ya utendaji kutoka muundo wa kiraia na kwenda katika muundo wa kijeshi.
Na. Hamis Dambaya- Mlele Katavi
0 Maoni