Kamishna wa Uhifadhi - Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Musa Nassoro Kuji, jana tarehe 23.01.2025 alifanya ziara ya kikazi katika Hifadhi ya Taifa Serengeti kwa lengo la kukagua shughuli za uhifadhi na utalii zinazotekelezwa ndani ya hifadhi hiyo.
Katika ziara hiyo, Kamishna Kuji alipokelewa na wenyeji
wake ambao ni Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Izumbe Msindai, Kamanda
wa Kanda ya Magharibi na Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Stephano Msumi, Mkuu wa
Hifadhi ya Taifa Serengeti.
Kamishna Kuji alifanya kikao na Maafisa na Askari wa
Uhifadhi wa Hifadhi ya Taifa Serengeti na kujadili masuala mbalimbali ya
uhifadhi na utalii ikiwemo changamoto za kiutendaji na mikakati ya kutatua
changamoto hizo.
Akiongea na Maafisa na Askari Uhifadhi hao, Kamishna Kuji
aliwapongeza Menejimenti ya Kanda ya Magharibi na Hifadhi ya Taifa Serengeti
kwa kazi nzuri inayoendelea kufanyika hasa katika eneo la uhifadhi na utalii.
Kamishna Kuji aliosema, “Nitumie fursa hii kuwapongeza
sana Serengeti kwa jitihada za kuimarisha uhifadhi na utalii na juhudi zenu
zimefanikisha kuchangia 54% ya mapato yaliyokusanywa na Shirika kwa kipindi cha
Julai 2024 hadi Desemba 2024, Hongereni sana”.
Maafisa na Askari wa Hifadhi ya Taifa Serengeti
walifurahishwa na ujio wa Kamishna huyo, nakuahidi kufanya kazi kwa bidii ili
kuleta matokeo chanya katika uhifadhi kwa kutokomeza ujangili na kutoa huduma
bora kwa wageni ili wanapoondoka baada ya utalii wao warudi tena kwa mara ya
pili au zaidi.
Kamishna Kuji yupo katika ziara za kawaida za kukagua
utendaji kazi na maendeleo katika vituo vilivyopo kanda ya magharibi, leo
Januari 24, 2025 anatarajia kufanya ziara yalipo Makao Makuu ya Ofisi za Kanda
ya Magharibi zikizopo wilayani Bunda katika mkoa wa Mara.
Na. Philipo Hassan - Serengeti
0 Maoni