Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Shirika la
Utalii Duniani la Umoja wa Mataifa (UN Tourism) zimesaini mkataba wa
makubaliano utakaoifanya Tanzania kuwa mwenyeji wa Kongamano la Pili la Kikanda
la Utalii wa Vyakula la Shirika la Umoja wa Mataifa (The 2nd UN Tourism
Regional Forum on Gastronomy Tourism for Africa) linalotarajiwa kufanyika
jijini Dar es Salaam Machi 11 hadi 13,
2025.
Hafla ya utiaji saini imefanyika kati ya Waziri wa
Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) na Katibu Mkuu wa
Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani (UN Tourism), Zurab
Pololikashvili katika kikao kilichofanyika Makao Makuu ya Shirika la Utalii
Duniani la Umoja wa Mataifa jijini
Madrid, Hispania leo Januari 24,2025.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Chana amesema
Tanzania inafuraha kuwa mwenyeji wa kongamano hilo linalotarajia kukutanisha
washiriki zaidi ya 300 kutoka mataifa mbalimbali duniani na kwamba kupitia
kongamano hilo Tanzania itajifunza kutoka mataifa hayo namna wanavyofanya katika kukuza utalii wa
vyakula.
“Kupitia Kongamano hili tunataka kuwajengea uwezo wapishi
wetu jinsi ya kutengeneza aina tofauti za vyakula ili watalii wanapokuja waweze
kufurahia vyakula vya nyumbani kwao lakini pia tunahitaji kuona ni fursa gani
zitakazotokana na kongamano hilo ili tuweze kujifunza utangazaji utalii wa
vyakula,” Mhe. Chana alisisitiza.
Mhe. Chana amefafanua kuwa Tanzania na UN Tourism
zimekuwa zikishirikiana katika masuala mbalimbali kwa lengo la kukuza utalii.
“Miongoni mwa maeneo tunayoomba ushirikiano kwa sasa ni
katika masuala ya sera na ukuzaji ujuzi, Rasilimali Watu na Mpango Mkakati wa Kukuza Utalii” alisema Mhe.
Chana.
Katika hatua nyingine, Mhe. Chana alisema Tanzania
inatambua na kuthamini jukumu muhimu la Shirika la Utalii Duniani la Umoja wa
Mataifa (UN Tourism) katika kuunda sera za kimataifa za utalii,kukuza utalii
endelevu na kukuza ukuaji wa uchumi.
Naye, Katibu Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la
Utalii Duniani (UN Tourism), Zurab Pololikashvili alisema kuwa Shirika la
Utalii Duniani limelenga kuitangaza Afrika kama sehemu ya utalii inayofikika
sambamba na kutangaza utalii wa vyakula.
Katika kufanikisha kongamano hilo, Bw. Pololikashvili
amependekeza kwa Tanzania kutumia njia zote za
mawasiliano ili kulitangaza kongamano hilo ikiwa ni pamoja na kutumia
watu maarufu wenye ushawishi katika jamii na kuwatumia wapishi wa vyakula
mbalimbali vya kiafrika.
“Pia ningeiomba Tanzania kuhakikisha zoezi la upatikanaji
wa viza pamoja na usafiri wa anga kwa ujumla linakuwa rafiki kwa waombaji
wanaotarajia kusafiri kuja kwenye kongamano hilo,” amesisitiza Pololikashvili.
Mkutano huo umehudhuriwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii
Tanzania, Mhe. Balozi Ramadhani Dau, Balozi wa Tanzania nchini Hispania, Mhe.
Balozi, Ali Jabir Mwadini, Mkurugenzi wa Utalii, Wizara ya Maliasili na Utalii,
Dkt. Thereza Mugobi, Mjumbe wa Bodi ya TTB, Said Kamugisha na Afisa Balozi,
Amos Tengu na sekretarieti ya Shirika la UN Tourism.
Na Mwandishi Wetu- Madrid, Hispania
0 Maoni