Leo Januari 30, 2025 mkoani Geita, maelfu ya waombolezaji
wamejitokeza kuaga miili ya wanafunzi saba wa Shule ya Sekondari Businda
iliyopo wilayani Bukombe waliofariki kwa kupigwa na radi mnamo tarehe 27
januari, 2025.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati ambaye pia ni Mbunge
wa Jimbo la Bukombe, Mhe. Dkt. Doto Biteko ameongoza shughuli za kuaga na
kukabidhi ubani kwa wafiwa huku akiwataka kuwa wavumilivu hasa kipindi hiki cha
majonzi.
Ametoa pole kwa wazazi, walezi ndugu wa watoto pamoja na
wanafunzi wa Businda kwa kuondokewa na wapendwa wao na wanajamii wa Businda
Sekondari kwa jitihada na utoaji wa huduma wakati wa tukio hilo.
“Imeandikwa kwamba shukuruni Mungu kwa kila jambo, Mungu
ametukutanisha leo katika hali ya majonzi. Tukio hili litukumbushe kutenda mema
wakati wote na tuamini kwamba Mungu ndiye mwenye uweza. Kipekee ningetamani
kuwataja Madaktari wote kwa majina kutokana na msaada mkubwa walioutoa lakini
itoshe kusema asantekwa kazi kubwa mliyoifanya,” amesema Dkt. Biteko.
Amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.
Samia Suluhu Hassan baada ya kupokea taarifa za msiba huo mzito amekuwa
akifuatilia kwa karibu na kutoa maelekezo kwa ajili ya kuzifariji familia za
wafiwa, wana Bukombe na Taifa kufuatia kuondokewa na vijana waliokuwa katika
safari ya kutafuta elimu.
“Rais Samia amegharamia msiba pamoja na kutoa ubani kwa kila
familia za wafiwa pamoja na kugharamia usafirishaji wa miili ya wanafunzi
wawili kwenda Chato, Geita na Karatu mkoani Arusha kwa mazishi.”
Viongozi mbalimbali wa dini wamewapa faraja wafiwa na kusema
msiba haujawahi kuzoeleka lakini kwa mapenzi ya Mungu atakuwa mfariji wao.
Viongozi hao wamewataka wanadamu kujipanga wakati wote kwa
kuwa hawajui ni wakati gani utafikwa na umauti kutokana na fumbo aliloliweka
Mwenyezi Mungu.
Aidha, wamemwomba Mungu awape uvumilivu viongozi katika
kipindi hiki cha majonzi.
Wanafunzi hao saba waliokuwa wakisoma kidato cha tatu
walikuwa na umri kati ya miaka 16 na 18, walikutwa na umauti kwa kupigwa na
radi wakati wakiendelea na masomo darasani.
Waliofariki ni Erick Emmanuel Akonaay (17), Nikas Paul
Tompoli (18) Gabriel Daud Makoye (17), Doto Marco Masasi (18), Asteria Reonard
Mkina (16), Peter Nkinga Manyanda (17) na Erick Martine Bugalama (16).
Awali, Mkuu wa Shule ya Sekondari Bulangwa, Theodora James
Mushi amesema wanafunzi hao walipatwa na
umauti wakiwa katika harakati za kusaka elimu.
Wanafunzi wanne kati yao walifariki papo hapo na wengine
watatu walifariki wakati wakipatiwa matibabu katika Hospitali na vituo
mbalimbali vya Afya.
Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Mhe. Paskazi Mragili ameishukuru Idara ya afya kwa utayari na uharaka wa utoaji huduma kwa wanafunzi wote 138 ambapo wanafunzi 89 waliathirika moja kwa moja na wengine waliruhusiwa kurudi nyumbani. Majeruhi wote wameruhusiwa na wale waliopata majeraha wanaendelea kutibiwa wakitokea nyumbani.
Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati


0 Maoni