Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Hassan
Abbas amewahamisisha Wataalamu wa utafiti wa Taasisi ya Utafiti wa Misitu
Tanzania (TAFORI), kuandaa miradi mbalimbali ya utafiti yenye kuleta maendeleo
chanya ndani ya Taasisi na katika sekta ya Misitu na ufugaji Nyuki.
Ameyasema hayo wakati akizungumza na Menejimenti ya
Utumishi wa Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) jana wakati
alipofanya ziara yake katika Taasisi hiyo kwaajili ya kuipongeza Taasisi kwa
mchango mkubwa wanaoutoa kupitia shughuli za kiutafiti na kusikiliza changamoto
zinazoikabili Taasisi hiyo.
Alisema, ili kukabiliana na changamoto mbalimbali za
Taasisi ni vyema kwa Taasisi kupitia wataalamu wake ikaanda miradi ya kimkakati
yenye kuleta maendeleo kwenye Taasisi na katika sekta ya Misitu na ufugaji
Nyuki ili kukuza pato la Taifa.
Dkt. Abbas alisema, Taasisi kupitia watafiti wake inahaja
ya kuongeza uzoefu kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya Misitu na ufugaji
Nyuki ndani na nje ya nchi pamoja na Taasisi na Mamlaka zilizoko chini ya
Wizara ya Maliasili na Utalii, kwa kufanya ziara mbalimbali ili kupata ujuzi na
maarifa utakaoongeza ufanisi katika utendaji kazi ndani na nje ya Taasisi.
Alisema, Taasisi inatakiwa kuwekeza katika mashamba
makubwa ya Misitu yatayotumika kwa ajili ya shughuli za kiutafiti na kuweza
kuanzisha biashara zitakazoleta maendeleo katika Taasisi na taifa kwa ujumla.
Hata hivyo, Katibu Mkuu ameitaka TAFORI kutatua kero na
changamoto zinazowakabili wananchi hapa nchini kwa kutoa elimu na mafunzo
kupitia tafiti wanazozifanya katika sekta ya Misitu na ufugaji Nyuki.
0 Maoni