Baraza la Wafanyakazi la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa
Serikali limekutana na kufanya kikao kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali
yatakayosaidia kurahisisha utendaji kazi na kutoa huduma bora zaidi za kisheria
kwa wananchi.
Kikao hicho kimefanyika jana katika Chuo cha Uongozi cha
Mwalimu Nyerere kilichopo Kibaha Mkoani, Pwani kwa kuwashirikisha wajumbe
kutoka Divisheni, Vitengo na wajumbe wa TUGHE kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu
wa Serikali.
Akizungumza wakati wa kikao cha Baraza hilo, Mwanasheria
Mkuu wa Serikali, Mhe, Hamza S. Johari, amesema kuwa lengo la kikao hicho ni
kufanya tathmini ya utendaji kazi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali
pamoja na kujadili na kuzipatia ufumbuzi changamoto mbalimbali ili kuleta
ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya Ofisi.
“Tumekutana kwenye kikao hiki cha Baraza na kupitia kwa
pamoja changamoto zetu hasa suala la mafunzo kwa Mawakili wetu, wapate mafunzo
katika kiwango kinachohitajika, na namna tunavyoweza kutumia TEHAMA hususan
mfumo wetu wa OAG - MIS katika kuboresha utoaji wa huduma zetu,” amesema
Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Aidha, Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema kuwa ni wazi
kuwa mwaka uliopita Ofisi ya Mwanasheri Mkuu wa Serikali wamefanya vizuri
katika eneo la utoaji wa huduma za ushauri wa kisheria ikiwemo uanzishwaji wa
Kliniki za Ushauri wa Kisheria ambazo zimeendelea kutolewa bure kwa wananchi
katika maeneo mbalimbali nchini.
“Kwa mwaka uliopita tumeweza kuanzisha Kliniki za
Kisheria tukiwa na lengo la kusogeza huduma za kisheria kwa wananchi katika
maeneo yao wanayoishi, na hivi sasa huduma hii tunaendelea kuitoa kwa wananchi
wa mkoa wa Kilimanjaro,” amesema Mhe. Johari.
Kwa upande wake Mgeni Rasmi katika ufunguzi wa kikao cha
Baraza la Wafanyakazi la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Katibu Mkuu wa
Wizara ya Katiba na Sheria Bw. Eliakim Maswi, ameipongeza ofisi ya Mwanasheria
Mkuu wa Serikali kwa namna ambavyo wamekuwa wakitekeleza majukumu yao, sambamba
na kuitisha kikao cha Baraza la Wafanyakazi kujadili masuala mbalimbali
yanayohusu ofisi hiyo.
Katika hatua nyingine Bw. Maswi ametoa wito kwa Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuendelea kutoa mafunzo kuhusu Upekuzi wa Mikataba
kwa Mawakili wa Serikali ili kuhakikisha wanaendelea kusimamia vizuri mikataba
ya Serikali kwa maslahi mapana ya Taifa.
“Wito wangu kwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ni
kuendelea kutoa mafunzo ya upekuzi wa Mikataba kwa Mawakili wa Serikali ili
kuendelea kuboresha utendaji kazi wa Mawakili na Wanasheria wetu katika
kusimamia Mikataba mbalimbali ambayo ina maslahi mapana kwa nchi,” amesema Bw.
Maswi.
Awali akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho,
Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Samwel Maneno, amesema katika kipindi
cha mwaka 2024/2025 Jumla ya mikataba 1,799 ilifanyiwa upekuzi ambapo kati ya
hiyo mikataba 1,639 ya manunuzi, 120 imehusu fedha,mkataba (1) kuhusu Maliasili
na 39 ni ya ushirikiano wa Kimataifa.
Naye Mwenyekiti wa TUGHE tawi la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu
wa Serikali, Bi. Zella Rwemanyira Ametoa rai kwa watumishi wa ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili waweze
kuendana na dhana ya Weledi na Ubora.
“Natoa rai kwa Watumishi wenzangu wa Ofisi ya Mwanasheria
kuendelea kuchapa kazi kwa bidi ili tuendane na dhana ya Weledi na Ubora,” amesema Bi. Zella.
0 Maoni