WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema kuwa Wilaya ya Ruangwa
imepiga kasi kubwa ya maendeleo ambayo imewawezesha wakazi wa Wilaya hiyo
kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Amesema kuwa Wilaya hiyo changa ilikuwa na changamoto nyingi
kwenye Sekta ya Elimu, Afya, Kilimo, Miundombinu ikiwemo barabara, maji, Umeme,
Uwekezaji na hata kwenye michezo “Changamoto hizi zilitufanya tuje na kaulimbiu
ya “Ruangwa kwa Maendeleo Inawezekana, na sasa imewezekana”
Ametoa kauli hiyo jana (Jumapili, Desemba 29, 2024) wakati
alipozungumza na mamia ya Wakazi wa kijiji ya Mbekenyera, wilayani Ruangwa
mkoani Lindi.
Amesema kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa na
mchango mkubwa katika maendeleo ya wilaya hiyo kutokana na fedha ambazo amekuwa
akitoa zilizowezesha kutekeleza miradi hiyo ya kimkakati.
Akizungumza kuhusu Sekta ya Elimu Mheshimiwa Majaliwa
amesema kuwa Wilaya ya Ruangwa ilikuwa na vijiji vichache kati ya tisini
vilivyokuwa na shule za msingi lakini hivi sasa kila kijiji kina shule ya
msingi “Na tunaendelea kujenga kwenye vitongoji.”
“Kwa upande wa shule za sekondari tumemaliza kata zote
kujenga shule za Sekondari kwenye Wilaya hii na tunachokifanya sasa ni kuongeza
shule kwenye kata zenye msongamano mkubwa na hapa Mbekenyera tulikuwa na shule
ya Tarafa, lakini baada ya kuona kuna msongamano wa wanafunzi, tumejenga shule
nyingine pale Mkutingombe.”
Aidha, Amesema kuwa Sekta ya Afya katika wilaya hiyo
imeimarika kwa kiasi kikubwa kutokana na ujenzi wa Zahanati, Vituo vya Afya
pamoja na ujenzi wa hospitali ya wilaya ambayo inauwezo wa kutoa hadi huduma za
kibingwa.
Ameongeza kuwa Wilaya hiyo imefanikiwa kujenga mtandao wa
barabara za lami katika maeneo mbalimbali na mpango wa kuendelea kujenga
barabara za lami unaendelea “Itakuja barabara ya kutoka Masasi kwenda
Kiranjeranje, na sasa Masasi kwenda Nachingwea mkandarasi yupo, Ruangwa kwenda
Nachingwea Mkandarasi yupo na ameanza kazi na tunajenga kilomita 21 kutoka
Ruangwa mjini mpaka Namichiga kwa kiwango cha lami.”
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa alizungumzia sekta za, kilimo,
maji na uwekezaji na kusema kuwa kazi kubwa imefanyika na Serikali inaendelea
kuziwekea mikakati endelevu sekta hizo “Kwenye sekta ya nishati, tumeshapeleka
umeme kwenye vijiji vyote na sasa tunaenda kwenye mradi wa vitongoji, ndugu
zangu wananchi, tumeshapeleka laini, ni wakati wenu sasa kuvuta umeme.”
Awali, Mheshimiwa Majaliwa alitembelea kiwanda cha kubangu
korosho cha Naunambe Cashewnuts kinachomilikiwa na Muwekezaji Mzawa Bw. Juma
Chambone na kina thamani ya Shilingi milioni 250. Kiwanda hicho kipo katika
kijiji cha Mbekenyera.
Pia Mheshimiwa Majaliwa aligawa vifaa vya muziki vyenye thamani ya shilingi milioni 20 kwa bendi ya Mkurupuko Jazz bendi iliyopo kwenye kijiji cha Mbekenyera.
0 Maoni