Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa Kushirikiana na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), wamezindua mpango wa kuwapatia chanjo dhidi ya Virusi vinavyosababisha Homa ya Ini (Hepatitis B Vaccine) kwa wafanyakazi 100 na wanafunzi 500 wa MUHAS wanaofanya mafunzo kwa vitendo hospitalini hapo.
Akizindua mpango huo leo Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali
ya Taifa Muhimbili (MNH) Prof. Mohamed Janabi ambaye pia ni Mshauri wa Rais wa
Masuala ya Afya na Tiba amesema lengo ni Kupunguza maambukizi ya Virusi vya
Homa ya Ini miongoni mwa wafanyakazi na wanafunzi wanaohudumia katika idara
mbalimbali, hasa wale wanaofanya kazi katika mazingira hatarishi kama
hospitali.
“Takwimu za Shirika la Afya Duniani zinasema wastani watu
3500 wanafariki duniani kutokana na matatizo yanayohusiana na Homa ya Ini.
Hivyo, ni muhimu kuwa na kinga dhidi ya ugonjwa huu, hasa kwa wafanyakazi wa
afya wanaokutana na hatari ya kupata maambukizi kupitia damu na majimaji ya
mwili,” alisema Prof. Janabi.
Prof. Janabi ameeleza kuwa mwaka huu, Hospitali ya Taifa
Muhimbili imefanya uchunguzi wa magonjwa mbalimbali kwa wafanyakazi wake,
ikiwemo saratani ya shingo ya kizazi, saratani ya matiti, na saratani ya tezi
dume kwa lengo la kugundua magonjwa haya katika hatua za awali, kwani kinga ni
bora kuliko tiba.
Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Serikali ya Wanafunzi MUHAS
Bw. Enock Sichone amesema mpango huo wa chanjo ya Homa ya Ini ni fursa muhimu
kwa wanafunzi wa afya, hasa kwa wale wanaofanya kazi wodini na kuhudumia
wagonjwa.
“Tunaushukuru uongozi wa MNH chini ya Prof. Janabi,
ambaye amekuwa mwepesi kutusaidia kila tunapomhitaji. Haya yote yanafanyika kwa
sababu ya umuhimu mkubwa wa kinga, lakini pia ni matokeo ya uongozi madhubuti
wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mh. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye
ameweka mifumo wezeshi na kuwekeza nguvu kubwa katika sekta ya afya,”
amefafanua Bw. Enock.
0 Maoni