Maonesho ya Kimataifa ya GITA MAHOTSAV yafunguliwa rasmi India

 

Shirika kongwe la Uhifadhi nchini (TANAPA) na Bodi ya Utalii (TTB) ni miongoni wa taasisi kutoka nchini Tanzania wanaoshiriki Maonesho ya Kimataifa ya Utalii na Utamaduni ya GITA MAHOTSAV yanayoendelea katika Mji wa Kurukshetra Jimbo la Haryana nchini India.

Maonesho hayo yalitanguliwa na maonesho ya kiimani/kidini kwa wananchi wa mji Mtakatifu wa Kurushektra yaliyoanza tarehe 28 Novemba, 2024 mpaka 4 Desemba, 2024 ambayo yalitoa nafasi kwa washiriki kutoka Tanzania kujifunza Imani ya watu wa India ambao wana Miungu takribani Milioni thelathini.

Ushiriki wa Tanzania ni kufuatia mwaliko wa Jamhuri ya watu wa India ambayo imekuwa na urafiki na uhusiano mzuri wa kindugu na kidiplomasia kwa muda wa zaidi ya miaka 60.

Hafla ya ufunguzi imehudhuriwa na Mheshimiwa Tabia Maulid Mwitta - Waziri wa Utalii Michezo na Utamaduni kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Mhe. Waziri akiwa na mwenyeji wake (Mkuu wa Jimbo la Haryana) na viongozi wa nafasi za juu kutoka Serikali ya India na Jimbo la Haryana walipata nafasi ya kutembelea Banda la Tanzania ambapo maelezo kuhusu vivutio, fursa za uwekezaji na Utalii yalitolewa vikiambatana na zawadi maalum kwa wageni kama sehemu ya ukarimu ambao nchi imejaaliwa.

Nchi ya India ni miongoni mwa masoko ya kimkakati kiutalii ambapo ushiriki wa Tanzania utasaidia kufikia idadi ya watalii milioni tano ifikapo 2025/2026. 

Aidha uwepo wa fursa za uwekezaji utatoa nafasi kwa watu wenye sifa na mitaji kuwekeza katika maeneo ya malazi na mazao ya Utalii kama wanavyoendelea kutangaza washiriki   hao.

Kwa upande wa Tanzania Maonesho hayo yanawakilishwa na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), TTB na maofisa kutoka ubalozi wa Tanzania nchini India.

Maonesho hayo yanayotarajiwa kufungwa rasmi kimataifa tarehe 11.12.2024 lakini kwa washiriki kutoka mataifa mbalimbali kuendelea na Maonesho ya kunadi bidhaa zao hadi Desemba 15, 2024 ili kutoka fursa zaidi kwa nchi washiriki kuendelea kupata masoko na kubasilishana uzoefu wa kibiashara.



Chapisha Maoni

0 Maoni