Watu
wasiojulikana wamemuua Isack Mallya (72) mkazi wa Kijiji cha Umbwe Onana, Kata
ya Kibosho Magharibi mkoani Kilimanjaro ambaye ni ndugu wa Mwenyekiti wa CCM
Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi, na kisha kuutelekeza mwili wake nje ya
nyumba yake.
Akithibitisha
kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa
amesema tukio hilo limetokea asubuhi ya Desemba 2, 2024 na kueleza kwamba polisi
wanafuatilia kujua waliohusika na mauaji hayo.
"Ni
kweli kumetokea tukio hilo la mauaji, ambapo huyu mzee amepigwa na kitu kizito
kichwani, tunafuatilia tukio hili ili kuwabaini waliohusika na mauaji
haya," amesema Kamanda Maigwa.
Kwa upande
wake Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi, ambaye ni ndugu wa
marehemu ameeleza kusikitishwa na ukatili aliofanyiwa kaka yake na kusema
wameliachia Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi ili kubaini waliohusika na sheria
ichukue mkondo wake.
"Isack ni
kaka yangu, ni mtoto wa baba yangu mkubwa, tumeishi wote mji mmoja na mahali
alipouawa ndipo nimekulia hapo, ni jambo la kikatili sana limefanyika katika
jamii, lakini naamini jeshi la polisi litafanya bidii kuchunguza matatizo
yaliyotokea na kuwatafuta waliohusika na jambo hili ili hatua za kisheria zichukue
mkondo wake," amesema Boisafi.
0 Maoni