Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezindua rasmi tuzo za
uhifadhi na utalii na kusisitiza kuwa Serikali itendelea kubuni mikakati ya
kuimarisha sekta ya Maliasili na Utalii kwa kuwa sekta hiyo ni nguzo muhimu ya
uchumi wa taifa.
Amesema hayo jana usiku alipozindua Tuzo za Uhifadhi na
Utalii katika Ukumbi wa Hoteli ya Mt. Meru jijini Arusha. Tuzo hizo zina lengo
la kuchochea ushindani kati ya wadau wa sekta ya maliasili na utalii nchini.
Amesema kuwa Sekta ya maliasili na utalii ni chanzo
kikubwa cha mapato ya taifa kwa kuwa inahusisha shughuli nyingi za kiuchumi.
“Sekta hii peke yake inachangia asilimia 21.5 katika pato
ghafi la Taifa ambapo asilimia 17.2 ni utalii, asilimia 4.3 ni misitu na nyuki,”
amesema Mhe. Majaliwa.
Aidha, amefafanua kuwa Sekta hiyo inachangia asilimia
30.9 ya mapato ya fedha za kigeni ambapo asilimia 25 yanatokana na utalii,
asilimia 5.9misitu na nyuki.
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa
juhudi za dhati na maono makubwa ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika
kuiendeleza Sekta ya Maliasili na Utalii yamesaidia kuongeza idadi ya watalii
wa kimataifa kwa asilimia 96 kutoka watalii 922,692 mwaka 2021 hadi watalii
1,808,205 mwaka 2023;
“Jitihada za Rais wetu Dkt. Samia zimesaidia pia
kuongezeka kwa mapato yatokanayo na Utalii wa Kimataifa kwa asilimia 68.2
kutoka dola za Marekani bilioni 2.0 mwaka 2021 hadi bilioni 3.4 mwaka 2023”.
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa ameiagiza Wizara ya
Maliasili na Utalii kuhakikisha inaweka vigezo vya wazi na vinavyojulikana vya
uteuzi na upokeaji wa tuzo.
“Vigezo hivyo, pamoja na mambo mengine viwe
vinavyozingatia ubora katika uhifadhi wa mazingira, huduma za utalii, usimamizi
wa hifadhi za wanyama, na uendelezaji wa maeneo ya utalii,” amesisitiza Mhe.
Majaliwa.
Naye, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Balozi Dkt.
Pindi Chana (Mb) amempongeza Rais Dkt. Samia kwa namna anavyojitoa katika
kuhakikisha Sekta ya Maliasili na Utalii inaendelea kukua kwa kasi.
Ameongeza kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii imekuwa na
mikakati mbalimbali ya kuimarisha uhifadhi na kuendeleza utalii ikiwemo kutumia
teknolojia mbalimbali pamoja kuendeleza Programu ya Tanzania – the Royal Tour
na kuibua mazao mapya ya utalii ili kuongeza idadi ya watalii na mapato
yatokanayo na shughuli za utalii.
0 Maoni