Jumla ya kaya 22 zenye watu 96 na mifugo 196 zilizokubali
kuhama kwa hiari kutoka ndani ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro zimepokelewa
rasmi katika Kijiji Msomera, Wilayani Handeni na kukabidhiwa makazi yao jana Desemba, 19 2024.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Handeni Albert
Msando, Katibu tarafa wa tarafa ya Sindeni Bw. Baraka Nkatura alisema kwamba
Serikali imejipanga vizuri kuhakikisha kwamba wananchi hao waliokubali kuhama
kwa Hiyari wanapatiwa huduma bora kama walivyoahidiwa.
“Baada ya kupokelewa nipende kuwahakikishia kuwa Serikali
imejipanga vizuri na vitu ambavyo mliahidiwa kuwa matavikuta Msomera viko
tayari. Mtapatiwa nyumba iliyojengwa kwenye eneo lenye ukubwa wa hekari 2.5,
Shamba la Ekari 5, Pamoja na maeneo yaliyotengwa mahususi kwa ajili ya shughuli
za ufugaji,” alisema Baraka.
Baada ya kukabidhiwa nyumba, Bw. Samweli Koromo ambaye ni
mmoja wa wananchi waliopokelewa Msomera Alisema kuwa wamefurahi sana baada ya
kuona kwamba wana uwezo wa kumiliki nyumba za kisasa tofauti na ilivyokuwa huko
Hifadhini ambako sheria za uhifadhi zilikuwa haziruhusu kufanya ujenzi wa
makazi bora ya kudumu.
“Nimefurahi sana nimepata Nyumba nzuri kwani kule
Ngorongoro tulikuwa hatuwezi kujenga wala kufanya shughuli za maendeleo, na pia
tumefika msimu wa mvua hivyo nitaanza kufanya maandalizi kwa ajili ya kilimo,”
alisema Samwel.
Kwa upande wake Bi. Esther Naftal ambaye kwa sasa ni
mkazi wa Msomera akitokea Ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro takriban miaka mitatu
iyopita, alisema kwamba wanafarijika kuona ndugu zao wanaendelea kupata
mwitikio wa kujiandikisha na kuhama kwa hiari kuja Msomera.
“Sisi tuliokuja mwazoni tumeshaona mazuri ya Msomera kwa
sasa tuna chakula cha kutosha baada ya kulima, tumeanzisha biashara, Watoto
wetu wanasoma shule, kwa ujumla maisha yetu yamekuwa bora zaidi. Wito wangu kwa
ndugu zetu waliobaki Ngorongoro wajiandikishe ili waweze kunufaika na furasa
hii tuliyopewa na Serikali,” alisema Esther.
Serikali kupitia Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro
inaendelea na zoezi la utoaji Elimu, uandikishaji na uhamishaji wa wananchi
wanaohama kutoka ndani ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro kwa hiari kuelekea
Msomera na maeneo mengine waliyochagua wenyewe.



0 Maoni