Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule ametoa
wito kwa wananchi wa Mkoa wa Dodoma na mikoa ya jirani kutumia fursa ya kununua
hisa zilizopo katika Hatifungani ya Miundombinu ya Barabara (Samia
Infrastructure Bond) kwaajili ya kuendeleza ujenzi wa miradi ya miundombinu ya
barabara za wilaya zinazosimamiwa na TARURA.
Ametoa wito huo wakati wa utoaji elimu ulioenda sambamba
na zoezi la uuzaji hisa za hatifungani hiyo kwa wadau mbalimbali wa mkoa wa
Dodoma na mikoa jirani katika ukumbi wa Mabele mkoani Dodoma.
“Ni mara chache sana kukutana na kujadili fursa za
uwekezaji, jambo hili ambalo ni muhimu kwenye maisha yetu tumekuwa hatulipi
kipaumbele, leo hii serikali na taasisi binafsi zinaungana katika suala la
maendeleo ya nchi yetu, CRDB na TARURA wametukutanisha hapa ili tuwekeze katika
Hatifungani ya Samia katika ujenzi wa barabara, naamini mapato yatakayopatikana
ya mauzo ya hatifungani hii yatasaidia kwa kiasi kikubwa kutekeleza miradi ya
barabara nchini hivyo nawasihi watu wengi tujitokeze kuwekeza katika
hatifungani hii”.
Katika hafla hiyo, Mhe. Senyamule alikusanya shilingi
Bilioni 1.5 kutoka kwa wadau mbalimbali ambapo ametoa wito kwa wadau wengine
kuendelea kuwekeza katika hatifungani hiyo ambayo faida yake inatoa riba ya
asilimia 12 kwa mwaka, inayolipwa kila robo mwaka ndani ya kipindi cha miaka
mitano.
Amesema hatifungani hiyo ina lengo la kukusanya fedha
zitakazowasaidia wakandarasi wazawa ili kuhakikisha barabara zinajengwa kwa
wakati lakini inatoa fursa kwa wawekezaji kupata faida kutokana na fedha
wanazoweka yaani unashiriki kujenga nchi huku unapata faida kutokana na mtaji
uliowekeza, amefafanua Mhe. Semanyule.
Kwa upande wake, Vivian Komu Mwenyekiti wa Bodi wa
Wakandarasi mkoani Dodoma amesema wao fedha hizo za hatifungani ya miundombinu
ya Samia zitawasaidia wakandarasi kutekeleza majukumu yao ya miradi hasa wakati
ambao serikali inakuwa haina fedha.
Hatifungani ya Samia inatolewa na Benki ya CRDB kwa ajili
ya kufadhili miradi muhimu ya miundombinu nchini ambapo kiasi cha shilingi
Bilioni 150 kinatarajiwa kukusanywa kupitia Hatifungani hiyo kwa ajili ya
kuendeleza ujenzi wa barabara chini ya TARURA ili kuongeza mtandao wa barabara
za vijijini na mijini, kuhakikisha ujenzi na ukarabati wa barabara unafanyika
kwa wakati na kusaidia kukabiliana na mahitaji ya dharura ya ujenzi na
ukarabati wa miundombinu unaosababishwa na uharibifu wa mvua
kubwa na mafuriko.



0 Maoni