Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto
Biteko amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Kagera Hajjat Fatma Mwassa kwa maandalizi
mazuri ya Kongamano la Uwekezaji mkoani humo litakaloibua fursa za uwekezaji na
kukuza uchumi wa mkoa.
Dkt. Biteko ametoa pongezi hizo leo Desemba 19, 2024
mkoani Kagera wakati akizungumza katika Tamasha la Pili la Uwekezaji la mkoa
huo ikiwa sehemu ya Wiki ya Ijuka Omuka (Kumbuka Nyumbani).
“Nawapongeza waandaaji wa Kongamano hili na kama kuna
watu wamekuja kuwekeza hapa napenda kuwapongeza wale mlioitikia wito tangu
kwenye kongamano la kwanza na kuja kuwekeza hapa,” amesema Dkt. Biteko.
Amesisitiza “Maombi yangu baada ya mkutano huu waje
wengine kuwekeza na tutumie fursa hii ya uwepo wa mkoa huu kijiografia na
kutumia fursa zilizopo.”
Aidha, amewaasa wananchi wa Mkoa wa Kagera kuunga mkono jitihada
za Mkuu wa Mkoa na kumpa ushirikiano wa kutosha katika kutekeleza majukumu
yake.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Innocent Bashungwa
amesema chinbuko la Tamasha hilo ni maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania aliyeta ifanyike tathmini ili kujua sababu za kudorora kwa uchumi na
maendeleo ya Mkoa wa Kagera. Amesema mnamo mwaka 2022 wadau walikutana na
kuainisha chanzo cha mkwamo kama mkoa.
“Wananchi wa Kagera tuna bahati ya kupata ushirikiano
mkubwa kutoka kwa Rais Samia na utashi wake wa kisiasa kuhusu mkoa wetu kutupa
miradi mbalimbali ya maendeleo na hivyo inatupa fursa zaidi ya kukuza uchumi
wetu,” amesema Mhe. Bashungwa.
Ameendelea kueleza kuwa sababu za kijigrafia kwa mkoa wa
Kagera pia zinauweka katika nafasi ya kimkakati kuleta maendeleo
"Kijiografia tunamshukuru Mungu mkoa wetu upo eneo la kimkakati na tuna
rasilimali watu wa kutosha hivyo tunawakumbusha wenzetu waliopo maeneo
mbalimbali ndani na nje ya nchi kukumbuka nyumbani licha ya majukumu yao huko
walipo.”
Mhe. Bashungwa ameishukuru Serikali kwa utekelezaji wa
miradi wa miradi mikubwa kama vile ujenzi wa daraja la Kigongo - Busisi ambalo
linatarajiwa kuzinduliwa mwezi Februari 2025, ujenzi wa barabara na pamoja na
kuzungumizia hitaji la mkoa wa Kagera kuingia kwenye Gridi ya Taifa.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mhe. Hajjat Fatma Mwassa amesema
kuwa lengo la Tamasha hilo la Pili la Uwekezaji la Mkoa wa Kagera ni kutoa
fursa kwa Serikali na mrejesho kwa wadau juu ya
mafanikio na mipango ya Serikali
kuhusu uchumi wa Mkoa huo.
Akielezea wasilisho lake la miradi na fursa zilizopo
mkoani humo, ametaja baadhi ya miradi inayoendelea kutekelezwa kuwa ni ujenzi
wa barabara za kimkakati zenye urefu wa km 265.4 zinazogharimu shilingi bilioni
340.49 na ujenzi wa madaraja matano utakaogharimu shilingi bilioni 45.2.
Miradi mingine ni vituo vinne vya umeme vilivyojengwa kwa
shilingi bilioni 163.
Katika sekta ya kilimo, Mhe. Mwassa amesema mkoa wake una
mikataba miwili ya miradi ya umwagiliaji inayogharimu shilingi bilioni 2.9.
Halikadhalika, mkoa huo unatekeleza miradi mikubwa ya
maji ya itakayogharimu kiasi cha shilingi bilioni 191 na kunufaisha zaidi ya wananchi 500,000.
Ameendelea kusema Mkoa huo umepakana na nchi jirani nne
na mikoa ya Kanda ya Ziwa Victoria na hivyo kuwahakikishia soko la uhakika wa
bidhaa.
Aidha, amewapongeza wawekezaji mkoani humo kwa kujenga
viwanda baada ya kuvutiwa na fursa zilizopo mkoani humo.
Pia, ametoa wito kwa wananchi kufuga samaki na dagaa kwa
vizimba na kuongeza thamani ili waweze kuuza nje ya nchi badala ya sasa ambapo
wanunuzi toka nje huenda kununua dagaa moja kwa moja kwa wafugaji wadogo.
Mhe. Mwassa amehamasisha uwekezaji wa hoteli mkoani humo
“Mikutano hii ya Jumuiya ya Afrika Mashariki haifanyiki hapa Kagera kwa sababu
hatuna uwezo wa kuhudumia idadi kubwa ya watu, mfano Polisi kutoka nchi hizi za
Jumuiya ya Afrika Mashariki walipenda kuja hapa kufanyia mkutano wao
haikuwezekana kwa sababu hatuna ukumbi wa kuhifadhi watu 3,000 kwa pamoja hivyo
walienda mahali pengine” amebainisha Mhe. Mwassa.
Vilevile, Mhe. Mwassa ameonesha kiu yake ya kuona uwanja wa ndege wa Omukajunguti
ukijengwa na kukamilika ili kutoa huduma kwa wananchi na kuchochea ukuaji wa
uchumi wa mkoa huo.
Mhandisi kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali
za Mitaa (TAMISEMI), Emannuel Mayanga amesema kuwa kupitia Miradi ya
Kupendezesha Miji (TACTIC) kwa manispaa ya Bukoba ni ujenzi wa barabara zenye
urefu km 10.75, uwekaji wa zaidi ya taa za barabarani zaidi 800 zitakazosaidia
kuangaza Bukoba wakati wa usiku, uboreshaji wa kingo za Mto Kanoni pamoja na
uboreshaji wa soko.
Kupitia tamasha hilo wadau na wawekezaji wamefanya
majadiliano kuhusu fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo mkoani humo.
Na. Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati



0 Maoni