Mtendaji
Mkuu wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mhandisi Victor
Seff amewataka Wahandisi wa TARURA
nchini kutoa ushauri wa kitaalamu kwa
wananchi na wadau wa maendeleo pindi
wanapofungua au kutengeneza barabara kwa nguvu zao kwa barabara ambazo hazipo
kwenye mtandao unaosimamiwa na TARURA.
Mhandisi
Seff ameyasema hayo wakati akiongea na watumishi wa TARURA Mkoni Mtwara katika
ziara yake ya kikazi ya ufuatiliaji wa miradi ya ujenzi na matengenezo ya
miundombinu ya barabara.
Amesema
wadau hao wanaojitolea kufungua barabara katika maeneo yao lengo lao ni zuri,
hivyo wanahitaji ushauri wa kitaalamu ili kuweza kutengeneza barabara
zitakazodumu kwa muda mrefu.
Naye Meneja
wa TARURA Wilaya ya Nanyamba Mhandisi Hussein Mwombeki amemweleza Mtendaji Mkuu
kuwa Wilaya hiyo ina ongezeko la barabara ambazo hazipo kwenye Mtandao wa
barabara za TARURA zilizofunguliwa na vikundi vilivyo kwenye Mradi wa TASAF.
Hata hivyo,
Mhandisi Seff ametumia fursa hiyo kuwapongeza watumishi wa TARURA Mkoa wa
Mtwara na Wilaya zake kwa kazi nzuri zilizoiletea sifa TARURA.
Aidha,
Mtendaji Mkuu huyo amewaasa watumishi kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili
kutoharibu sifa zinazopokelewa na Wakala.
Katika ziara
hiyo Mhandisi Seff ametembelea Ofisi za TARURA wilaya ya Masasi, Nanyumbu,
Tandahimba, Nanyamba pamoja na kukagua miradi ya ujenzi wa barabara
zilizoathirika na mafuriko ya mvua msimu uliopita.
Baada ya
kumaliza ziara yake Mkoani Mtwara, Mhandisi Seff anaelekea Mkoani Lindi kufanya
ufuatiaji wa kazi zinazofanywa na TARURA pamoja na kuongea na Watumishi Mkoani
humo.


0 Maoni