Wananchi 186
wenye maumivu makali wamejitokeza Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwenye
kambi maalum inayoendelea ambapo 25 kati yao tayari wametibiwa kupitia tiba
radiolojia na kuondokana na changamoto hiyo kupitia sindano za; goti, uti wa
mgongo kwenye pingili za uti wa mgongo, sindano za kuua neva zinazo husiana na
maumivu ya nyonga au mabega pamoja na matibabu ya maumivu ya tumbo
yasababishwayo na saratani ya kongosho.
Akizungumza
na vyombo vya habari leo Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa MNH Prof.
Mohamed Janabi amesema maumivu makali yanasababishwa na mambo kadhaa ikiwemo
kudhoofika kwa viungo vya mwili kutokana na umri, saratani, kusagika kwa diski
za pingili za mgongo , majeraha yaliyotokea muda mrefu uliopita n.k
Prof. Janabi
amesema kambi hiyo si tu imewanufaisha wagonjwa, pia imetumika kama jukwaa la
kipekee la kuhamisha ujuzi kwenda kwa wataalam wazalendo ambao wataendelea
kutoa matibabu hayo hatua kwa hatua na kuifanya huduma hiyo kuwa endelevu hapa
nchini.
Kwa upande
wake Prof. David Prologo, Bingwa Mbobezi kutoka Hospitali ya Emory Johns Creek
ya nchini Marekani aliyeongoza timu ya madaktari wabobezi, idara ya radiolojia
MNH, kitengo cha tiba radiolojia amesema anajivunia utalaam uliopo hususani
vifaa tiba vya kisasa na watalaam wabobezi ambao wameshirikiana kutoa huduma
hiyo.
Prof.
Prologo amekiri uwepo wa umahiri wa wataalam wa ndani wa kutoa matibabu hayo
kwa uendelevu wa huduma hiyo hata asipokuwepo.
Akihitimisha
mkutano huo, Prof. Janabi amemshukuru Prof. Prologo kwa kujitolea kwake
kuboresha huduma za afya katika taifa letu pamoja na taasisi ya Road2IR ambayo
siyo tu imechangia kuanzishwa kwa tiba radiolojia nchini bali imeendelea
kuratibu safari za wataalam wa tiba radiolojia kutoka sehemu mbalimbali duniani
hususani Marekani na Ulaya kuleta ujuzi wao nchini.

0 Maoni