Naibu Waziri
Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa mwaka 2015,
Tanzania iliunga mkono Ajenda ya Mpango wa Kimataifa wa Usalama wa Afya na
kuharakisha utekelezaji wa Sheria za Afya za Kimataifa ili kuzuia magonjwa ya
kuambukiza kusambaa kimataifa.
Kupitia
tathimini ya pamoja ya mwaka 2023 matokeo ya maendeleo ya Tanzania katika suala
hilo inaonyesha hatua kubwa ambapo mwaka 2016 imedhihirika azma imara ya
Serikali katika kutekeleza Sheria za Afya za Kimataifa kwa kutumia njia moja
ikikubali uunganishaji wa afya ya binadamu, wanyama, na mazingira.
Dkt. Biteko
amesema hayo leo Novemba 13, 2024 katika ufunguzi wa Kongamano la 14 la
Kimataifa la Sayansi la Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Sayansi za Afya (CUHAS)
lililofanyika jijini Mwanza lenye kaulimbiu “Afya Moja na Usalama wa Afya wa
Kimataifa.”
Ametaja
jitihada zilizofanywa na Serikali za kuhuisha miongozo na mipango kazi ili
kutekeleza Ajenda ya Mpango wa Kimataifa wa Usalama wa Afya.
“Mwongozo wa Kitaifa wa Maabara na Usalama wa
Bioteknolojia, Ajenda ya Mpango ya Kazi wa Taifa wa Usalama wa Afya, Mpango wa Mkakati wa Afya
Moja (2022-2027), Mpango Mkakati wa Kitaifa wa Kudhibiti Usugu wa Vimelea vya
Magonjwa dhidi ya Dawa (UVIDA 2023-2028). Pamoja na kuhamasisha ukuzaji na
uendelezaji wa raslimali watu na kuchochea ushirikiano wa kisekta,” amesema
Dkt. Biteko.
Ameendelea kusema kuwa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kufanya jitihada za
kuhakikisha Usalama wa Afya wa Kimataifa hasa kwa kutoa ufadhili wa masomo na
mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu kwa lengo la kuongeza nguvu kazi kila
mwaka.
“Serikali ya
Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa, Dkt. Samia Suluhu Hassan,
inathamini mchango wa Chuo Kikuu cha
Kikatoliki cha Sayansi za Afya pamoja na Kituo cha Tiba cha Bugando kwa
ushirikiano na washirika wa ndani na kimataifa kwa kuwa mabingwa katika nyanja
mbalimbali za utafiti zinazohusiana na Usalama wa Afya wa Kimataifa,” ameeleza
Dkt. Biteko.
Ameongeza
“Pia Serikali inathamini mchango uliotolewa na Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha
Sayansi za Afya kuanzia mwaka 2007 hadi 2023, ambapo kimezalisha zaidi ya
wataalamu wa Afya 7,000 katika fani mbalimbali za tiba, dawa, uuguzi, maabara
na uchunguzi wa kiafya, na uchomaji wa mionzi ambao wamekuwa mabingwa katika
Usalama wa Afya ya Kimataifa.”
Aidha, Dkt.
Biteko ameipongeza CUHAS kwa kuandaa makongamano hayo ya kisayansi yanayojadili
masuala ya kisera ili kutatua changamoto zilizopo katika sekta ya afya na
kusema kuwa afya ya binadamu inakumbwa na matishio mengi ili kukabiliana nayo
ni lazima kufanya utafiti.
“Nawapongeza
kwa kuleta wataalamu kwa ajili ya kujadili masuala ya tiba, niwapongeze pia kwa
ugunduzi wa aina ya kirusi kinachoitwa Bugandosis ambacho kimebadilisha mfumo
wa tiba na kutoa mchango katika sekta ya afya.”
Fauka ya
hayo amempongeza Prof. Stephen Mshana kutoka Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha
Sayansi za Afya kwa kuwa mwanasayansi bora kwa mwaka 2024.
Kwa upande
wake, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Omary Kipanga
amemshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha sekta ya umma na
binafsi hususan katika elimu na afya, akitolea mfano kupitia mradi wa Elimu ya
Juu na Mabadiliko ya Uchumi (HEET).
Mradi ambao
umesaidia elimu ya juu na kuwezesha ushirikiano kati ya sekta ya umma na
binafsi ikiwemo kutoa ufadhili wa masomo kwa wafanyakazi wa Chuo Kikuu cha
Kikatoliki cha Sayansi za Afya.
Mhe. Kapanga
ameongeza kuwa Afya Moja inasisitiza kutafuta suhulu ya pamoja ya changamoto
ngumu za kiafya na kuwa Kongamano hilo linasaidia wataalamu, wanasayansi na
watunga sera kujadiliana kwa pamoja Usalama wa Afya.
“Ni
matumaini yangu tutanufaika kutokana na utaalamu na matokea ya tafiti zilizofanyika
awali na mikakati itakayosaidia kupunguza matishio ya afya, nakishukuru Chuo
Kikuu cha Kikatoliki cha Sayansi za Afya kwa kuandaa Kongamano hili,” amesema
Mhe. Kipanga.
Naye, Makamu
Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Sayansi za Afya Bugando (CUHAS), Prof.
Erasmus Kamugisha amesema kuwa kauli mbiu ya Kongamano hilo Afya Moja inalenga
kuleta muunganiko wa binadamu, wanyama na afya ya mazingira ambayo inaathiri
jamii, taifa na dunia katika kufikia matokeo bora ya afya.
Ameongeza
kuwa Kongamano hilo linalofanyika kila mwaka limehudhuriwa na takribani
washiriki 500 kutoka nchi mbalimbali duniani na litakuwa na tafiti za sayansi
150 zitakazojadiliwa kwa siku mbili.
Inaelezwa
kuwa tafiti mbalimbali zinazowasilishwa kupitia makongamano hayo zimeweza kushawishi
kubadilishwa kwa miongozo au sera za huduma za afya nchini ikiwemo mabadiliko
ya dawa.
Aidha, kwa
mwaka 2024 yamechapishwa jumla ya machapisho 271 kuhusu mada mbalimbali za
tafiti.
Na. Ofisi ya
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati

0 Maoni