TARURA yapongezwa ujenzi wa daraja la Mto Zimba wilayani Nkasi

 

Wananchi wa Kata za Chala na Ntuchi katika Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa wameipongeza Serikali kupitia Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa ujenzi wa Daraja la mawe la mto Zimba linalounganisha Kata za Chala na Ntuchi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi hao wameishukuru Serikali kwa kujenga daraja hilo ambalo limewasaidia kusukuma maendeleo yao na kumaliza usumbufu kwa kupita kwenye maji kila wanapotaka kusafiri kwenda maeneo mengine kwa ajili ya kufuata huduma mbalimbali za kijamii.

Bw. Oteli Mwambilija mkazi wa Chala, ameishukuru Serikali kwa ujenzi wa daraja hilo kwani limekuwa kiunganishi kikubwa kwa wakazi wa kata za Chala na Ntuchi na limerahisisha shughuli za maendeleo pamoja na shughuli za usafiri na usafirishaji.

“Tunaishukuru TARURA kwa ujenzi wa daraja hili, awali kipindi cha mvua mto huu ulikuwa unajaa sana maji na kusababisha kero kubwa kwa wananchi kuvuka kwenda ng’ambo ya pili, watu walikuwa wanavuka kwa shida, ng’ombe wetu walisombwa na maji na tulikuwa tunawakuta mto jirani wa Mfizi, kwakweli tunaishukuru Serikali kwa kujenga daraja hili kwa sasa tunavuka bila shida yoyote,” alisema.

Naye, Bw. Samuel Mayesha mkazi wa Chala alisema, baadhi ya vijana walitumia changamoto ya kukosekana kwa daraja katika mto huo kama fursa kwani walikuwa wanavusha watu kwa fedha, hapo awali watu walipoteza maisha kwa kukosa daraja lakini sasa hivi wananchi wanafurahia na daraja limesaidia kusafiri na kusafirisha mazao yao.

Kwa upande wake, Meneja wa TARURA Wilaya ya Nkasi Mhandisi Karilo Samson, alisema kuwa ujenzi wa daraja la mawe la mto Zimba lenye urefu wa mita 31 pamoja na barabara unganishi ya Chala-Ifundwa Km 11.8 limegharimu shilingi milioni 350.

“Barabara hii tumeifungua haikuwepo hapo awali na tumejenga madaraja (2) ambapo mojawapo ni hili daraja la mto Zimba kwa kutumia teknolojia ya mawe, baada ya kufungua barabara tunaendelea na matengenezo ili iweze kupitika majira yote, kwa sasa mkandarasi yupo “site” anaweka vifusi maeneo korofi yaliyokuwa na utelezi,” alisema.

Alisema, daraja hilo limekamilika na linatumika kwa ajili ya usafiri na usafirishaji wa bidhaa hasa mazao kutoka mashambani kwenda sokoni na amewataka wananchi kuhakikisha wanalitunza ili liweze kudumu na kutumika kwa muda mrefu.

Chapisha Maoni

0 Maoni