Tanzania yapanda viwango vya soka vya FIFA, Kenya yashuka

 

Tanzania imekuwa miongoni mwa nchi zilizofanya vyema katika viwango vya soko dunia vya  FIFA baada ya kupanda kwa nafasi sita kutoka nafasi ya 112 hadi 106, na kuipita nchi ya Kenya.

Mafanikio hayo ya Tanzania yamechangiwa na Taifa Stars kushikilia nafasi ya pili katika Kundi H nyuma ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na kufuzu kwa Fainali za Mataifa ya Afrika 2025.

Kwa upande wa Timu ya taifa ya Kenya ya mpira wa miguu Harambee Stars imeshuka kwa nafasi mbili katika viwango vya hivi punde vya Fifa vilivyotolewa Alhamisi na shirikisho hilo la soka duniani.

Timu ya taifa ya kandanda sasa iko katika nafasi ya 108, chini kutoka nafasi ya 106 iliyokuwa nayo Oktoba.

Kushuka huku kwa Kenya kunatokana na kushindwa kufuzu kwa Fainali za Mataifa ya Afrika 2025 na kuikosa michuano hiyo yenye hadhi ya juu zaidi barani.

Harambee Stars ilimaliza ya tatu katika Kundi J nyuma ya Cameroon na Zimbabwe kufuatia sare ya 1-1 dhidi ya timu ya taifa ya Namibia na sare tasa dhidi ya Namibia katika mechi mbili za mwisho za kufuzu mapema mwezi huu.

Kwa upande wa Uganda yenyewe imesalia na nafasi yake ya juu zaidi katika ukanda wa CECAFA licha ya kushuka kwa nafasi moja hadi 88 huku Morocco ikisalia kuwa nchi iliyo juu zaidi barani Afrika katika nafasi ya 14.

Nchi ya Argentina inasalia kuwa kikosi kinachoongoza juu kwenye viwango vya FIFA, huku Ufaransa na Uhispania zikihifadhi nafasi zao katika nafasi ya pili na ya tatu mtawalia.

Chapisha Maoni

0 Maoni