Mkurugenzi
Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Prof. Mohamed Janabi amesema
uongozi utaendelea kuboresha utoaji wa huduma katika Hospitali ya Muhimbili
Mloganzila ili wananchi wapate huduma bora na zinazokidhi matarajio yao.
Prof. Janabi
amebainisha hayo alipokuwa akizungumza na Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi
katika kikao chake cha 29 kinachofanyika Dar es Salaam ambapo mada mbalimbali
zimejadiliwa katika kikao hicho.
Amefafanua
kuwa kutokana na usimamizi mzuri na kuendelea kuboresha huduma kwa wateja
kwasasa malalamiko yaliyokua yakitolewa na wananchi yamepungua kwa kiasi
kikubwa na wananchi wana imani na hospitali hiyo.
“Katika
hospitali hii tumeweza kuondoa mtazamo mbaya juu ya Mloganzila kwamba mgonjwa
akifikishwa huku anakufa, sasa hivi wananchi wamerejesha imani na hii
inajidhihirisha wazi kwani idadi ya wagonjwa wameongezeka mfano katika wagonjwa
wa nje awali tulikua tunaona wagonjwa takribani 400 hadi 450 sasa tumefikia
wagonjwa 800 hadi 1000 kwa siku,” amefafanua Prof. Janabi.
Prof. Janabi
ameeleza kuwa Muhimbili Mloganzila imeendelea kuboresha na kuanzisha huduma
mpya za ubingwa bobezi ikiwemo upandikizaji wa nyonga na magoti, upandikizaji
figo, upandikizaji uloto, kupunguza uzito, upandikizaji wa meno kwa njia ya
kisasa. Huduma hizi pamoja na nyinginezo zimekuwa kivutio kikubwa kwa watu
wengi wa ndani na nje ya nchi na hivyo kupunguza rufaa za kwenda nje ya nchi
kwa ajili ya matibabu.
Hospitali ya
Mloganzila Ilikabidhiwa rasmi kwa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa usimamizi
mwaka 2018 ambapo tangu kipindi hicho maboresho makubwa yamefanyika ikiwa ni
pamoja na kusomesha wataalam, kuongeza idadi ya huduma pamoja kuboresha eneo la
huduma kwa wateja.
0 Maoni