Ndani ya kipindi cha miaka mitatu ya
awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, bajeti ya uboreshaji wa miundombinu ya barabara za TARURA
imeongezeka kutoka Shilingi Bilioni 275 hadi Shilingi Bilioni 710.
Hayo yameelezwa mwishoni mwa wiki na
Naibu Waziri OR-TAMISEMI, Mhe. Zainabu Katimba wakati wa utiaji saini mkataba
wa ujenzi wa Soko Kuu la Mwanga na Soko la Samaki la Katonga katika Manispaa ya
Kigoma.
Mhe. Katimba alisema kwamba ongezeko
hilo la bajeti ni sawa na asilimia 158.18 ambapo zinaenda kutekeleza miradi
mbalimbali nchini.
Aidha, alisema kuwa kutokana na mvua
kubwa zilizonyesha maeneo mbalimbali ya nchi na kusababisha madhara makubwa
kwenye miundombinu ya barabara kama vile mvua za El nino, kimbunga Hidaya, Mhe.
Rais Samia aliongeza Bajeti ya dharura ya TARURA kutoka Shilingi Bilioni 21
hadi kufikia Shilingi Bilioni 254.3 sawa na ongezeko la asilimia 1,110.9 ya
bajeti ya dharura.
“Mhe. Rais kwa kutambua kuwa barabara
hizi zinaunganisha jamii zetu kwa kutoa huduma mbalimbali za kijamii na
zinatumika kwenye usafirishaji wa bidhaa mbalimbali za biashara na kupelekea
kukuwa kwa uchumi wetu aliongeza Bajeti ya dharura ya TARURA.”
Aliongeza kusema kuwa Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikichukua hatua mbalimbali zenye lengo
la kuboresha maisha ya wananchi na mojawapo ya hatua zinazochukuliwa ni
kuboresha miundombinu ya usafiri na usafirishaji.
“Msingi wa maboresho haya ni
utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi 2020- 2025, kama inavyofafanuliwa
katika aya ya 57 ukurasa wa 82,” aliongeza Mhe. Katimba.
#Bajeti ya dharura nayo yaongezezeka
Na. Catherine Sungura- Kigoma
0 Maoni