Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa
Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewataka wadau wa sekta ya uziduaji kubainisha
fursa na changamoto zilizopo katika sekta hiyo, kujadiliana kwa uwazi na
kuambizana ukweli kuhusu hali halisi katika sekta hiyo.
Dkt. Biteko ameyasema hayo Novemba 5,
2024 Jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa Jukwaa la Uziduaji kwa Mwaka 2024
lenye kauli mbiu “Sekta ya Uziduaji, Maendeleo Endelevu na Mhamo wa Nishati
Tanzania.”
“Semeni kwa uwazi na kuambizana ukweli
ili kusukuma maendeleo kwa pamoja, mngejua kuhusu matishio ya dunia na siasa za
ulimwengu, dunia inapita katika misukosuko mingi ikiwemo mabadiliko ya tabia
nchi na matokeo yake ni ongezeko la idadi ya matetemeko ya ardhi katika maeneo
mbalimbali duniani hivyo katika majadiliano yenu, angalieni michango ya nchi,
visababishi na mahitaji yake,” amesema Dkt. Biteko.
Ametoa mfano kuwa tafiti zinaonesha
kumekuwa na ongezeko la idadi ya matetemeko ya ardhi kutoka tisa mwaka 1950
hadi matetemeko 51 miaka ya 1970 idadi ambayo imeongezeka kufikia 150 miaka ya
1990 jambo ambalo amelitaka Jukwaa la Uziduaji kujadiliana kwa kina kuhusu
mwelekeo wa halisi wa maendeleo ya Bara la Afrika kwa miaka ijayo.
“Wakati dunia ikiwa katika hatari
kubwa inayotokana na matumizi ya nishati isiyo safi na salama, tujadili mchango
wa mtu na nchi mojamoja ili kufikia maamuzi sahihi yatakayowezesha kuleta
maendeleo, kila mtu na mchango wake kulingana na hali yake mfano nchi kama
Marekani mtu mmoja kwa mwaka anatumia wastani wa mapipa 22 ya mafuta huku
wastani kwa nchi za Afrika ni matumizi ya pipa moja kwa mwaka,” amesema Dkt. Biteko.
Amesema kuwa Sekta ya Uziduaji kwa
ukubwa wake inajumuisha rasilimali za madini, mafuta na gesi ambazo ni muhimu
katika maendeleo ya Taifa. Kwa kuzingatia umuhimu wake Dira ya Maendeleo ya
Taifa ya mwaka 2025 iliainisha kuongeza kasi ya ukuaji wa sekta ya madini na
kuongeza mchango wake katika Pato la Taifa kwa asilimia 10 hadi kufikia mwaka
2025 na kwa sasa kuna uhakika wa kufikia kiasi hicho.
Dkt. Biteko ametaja jitihada
zinazofanywa na Serikali ambazo zimeendelea kuimarisha Sekta ya Nishati ikiwa
ni pamoja na uwezo wa mitambo ya kufua umeme iliyounganishwa katika mfumo wa
Gridi ya Taifa umeongezeka na kufikia Megawati 2,607.96 ikilinganishwa na
Megawati 1,605.86 zilizokuwepo mwaka 2021 ikiwa ni ongezeko la asilimia 62
ambalo limetokana na kukamilika kwa miradi mbalimbali ya kuzalisha umeme
nchini.
Aidha, ujenzi wa Bwawa la kuzalisha
umeme la Julius Nyerere lenye uwezo wa kuzalisha Megawati 2,115 ambapo
utekelezaji wake umefikia asilimia 99.21 na kwa sasa unazalisha MW 1,175.
Vilevile, Serikali imeendelea kuimarisha
miundombinu ya kusafirisha umeme kwa kujenga njia mpya za kusafirisha umeme
kufikia urefu wa kilomita 7,745.4 kutoka kilomita 6,111.27 zilizokuwepo mwaka
2021 ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 26.7. Aidha, njia za kusambaza umeme
zimeongezeka na kufikia urefu wa kilomita 187,817.3 ikilinganishwa na kilomita
153,988.49 za mwaka 2021, sawa na ongezeko la asilimia 21.9.
Naye, Waziri wa Madini, Mhe. Anthony
Mavunde amesema kuwa Serikali imeendelea kuimarisha sekta ya madini ikiwa ni
pamoja na kuongeza bajeti yake kwa mwaka hadi kufikia takribani shilingi
bilioni 200 pamoja na kufanya utafiti wa kina wa madini na kuongoza vyema
wachimbaji wadogo.
“Katika mwaka wa fedha 2023 wachimbaji
wadogo walichangia zaidi ya asilimia 40 katika Mfuko Mkuu wa Serikali na mwaka
huu tunajiandaa kuchangia shilingi trilioni 1, katika miezi mitatu tangu mwaka
kuanza tumevuka lengo kwa kuchangia bilioni 96,” amesema Mhe. Mavunde.
Ameongeza kuwa Tanzania ina madini ya
mkakati ya kutosha na kuwa inaandaa mkakati maalum utakaosaidia kuvuna madini
hayo mfano kinywe.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. David Mathayo amesema kuwa Kamati
yake imefurahishwa na uwazi na uwajibikaji unaofanyika katika masuala ya
uziduaji.
Aidha, ameishauri Serikali kuendelea
kuwasaidia wachimbaji wadogo wa dhahabu ili waendelee kuzalisha dhahabu kwa
njia salama kwa kuwaongezea mitaji na teknolojia ili waachane na matumizi ya
zebaki.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Haki
Rasilimali, Bw. Adam Anthony amesema kuwa Jukwaa hilo la uziduaji linakutanisha
wadau wa sekta kwa lengo la kujadiliana na kubadilishana uzoefu kuhusu masuala
ya uziduaji.
Na. Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na
Waziri wa Nishati



0 Maoni