MAMLAKA ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imeanza rasmi utekelezaji wa mikakati ya kuiendeleza na kuiandaa Hifadhi ya Makuyuni Wildlife Park iliyopo Mkoani Arusha kwa ajili ya kupokea wageni wengi zaidi kwa kuongeza mindombinu ya utalii hususani barabara, ujenzi wa mabwawa ya maji Kwa ajili ya wanyamapori na kuondoa mimea vamizi ndani ya eneo hilo.
Hayo
yamesemwa jana Novemba 24, 2024 na Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya
TAWA Dkt. Simon Mduma katika ziara ya wajumbe wa Bodi hiyo ya kukagua ujenzi wa
miradi ya maendeleo inayotekelezwa na TAWA ndani ya Hifadhi ya Makuyuni
Wildlife Park.
"Hifadhi
hii ni mpya ilikabidhiwa takribani mwaka mmoja uliopita na katika mchakato
wakuiendeleza na kuiandaa Kwa ajili ya kupokea wageni kulikuwa na umuhimu wa
kuongeza barabara kwenye maeneo haya ili wageni watakaokuwa wanatembelea eneo
hili wawe na wigo mpana wa kuiona mandhari nzuri sana ya eneo hili lakini
vilevile kutoa nafasi kubwa ya kuona vivutio ambavyo vipo kwenye hifadhi hii,"
amesema Dkt. Mduma.
"Leo
tumezunguka na tumeona maendeleo ya ujenzi wa barabara, ni kazi ambayo
inaridhisha, ni nzuri na ratiba ambayo ipo kwa makubaliano kwenye mikataba Kazi ya ujenzi wa barabara
inaendelea vizuri sana hilo tumeridhika nalo," ameongeza Mduma.
Dkt. Mduma amesema
kutokana na eneo la Makuyuni kukumbwa na changamoto ya ukame wakati wa kiangazi
kiasi cha kusababisha wanyamapori kutoka nje ya hifadhi hiyo na kwenda kwenye
makazi.ya watu, Bodi ya TAWA iliona umuhimu wa kujenga bwawa la kukusanyia maji
Kwa ajili ya wanyamapori, hivyo Bodi hiyo imefanya ukaguzi wa eneo
litakapochimbwa bwawa hilo na kuridhishwa nalo, na hivyo ujenzi wake utaanza
hivi karibuni kwakuwa mikataba imekwisha sainiwa tayari Kwa kuanza kazi hiyo.
Kwa upande
wake mjumbe wa Bodi hiyo Profesa Suzanne Augustino ameipongeza Menejimenti ya
TAWA na watumishi wote Kwa jitihada kubwa wanayoifanya kuboresha mazingira ya
Makuyuni Wildlife Park ikiwa ni pamoja na kufanyia kazi ushauri na maelekezo
yanayotolewa na Bodi hiyo inayoongozwa na Mwenyekiti wake Mej. Jen. (Mstaafu)
Hamis R. Semfuko.
Aidha
Profesa Suzanne ametanabaisha kuwa kutokana na kuendana na kasi ya Rais wa
awamu ya Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan
ambaye amekuwa Balozi wa utalii wa nchi yetu na uwekezaji wa miundombinu ya
utalii unaofanywa na TAWA, Makuyuni Wildlife Park ya miaka mitano ijayo haitakuwa kama inayoonekana leo badala yake
itakuwa Makuyuni yenye mabadiliko makubwa ambayo inafungua njia kwa watalii
wengi zaidi lakini pia Makuyuni yenye utofauti mkubwa na maeneo mengine yenye
vivutio vya utalii.
Naye
Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi ambaye pia ni Kaimu Kamanda wa Uhifadhi Kanda ya
Kaskazini ya TAWA Privatus Kasisi amesema Kitendo cha Serikali kuiamini TAWA na
kuikabidhi eneo hilo muhimu kumeipa chachu
na nguvu ya kuliendeleza na kulisimamia kwa ukamilifu ili kulifanya liwe bora
kwa manufaa ya wakazi wa Mkoa wa Arusha na Taifa Kwa ujumla.
Aidha Kasisi
amesisitiza kuwa TAWA itahakikisha inaongeza kasi ya uboreshaji wa miundombinu
ya eneo hilo ili kupata watalii wengi na mapato kwa muda mfupi hasa katika
mashindano ya AFCON ya mwaka 2027 ambapo Tanzania inatarajia kupokea wageni
wengi kutoka mataifa mbalimbali na Arusha ni moja ya miji ambayo itapokea
wageni hao.
Katika hatua
nyingine, Kamanda wa eneo la Makuyuni Wildlife Park Andrew Kishe amesema miradi
yote inayotekelezwa na TAWA ndani ya Hifadhi hiyo inagharimu zaidi TZS Billioni
moja ambayo inajumuisha barabara atakazopewa mkandarasi na zile
zinazotengenezwa Kwa kutumia vitendea kazi vya taasisi huku akibainisha kuwa
barabara zinazofunguliwa zina mrefu wa Kilometa 18.
Vilevile
miradi hiyo inajumuisha ujenzi wa geti kubwa la kisasa la watalii na bwawa la maji Kwa ajili ya wanyamapori ambapo
ujenzi wa miradi yote hiyo inatokana na fedha za ndani ya
taasisi ya TAWA.
Na. Beatus
Maganja- Arusha
0 Maoni