Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na
Utalii imeridhika na miradi mbalimbali
ya misitu na nyuki inayotekelezwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Mfuko wa Misitu na Chuo cha Mafunzo ya
Ufugaji Nyuki Tabora (BTI) na kupongeza
kwa kazi nzuri inayofanyika.
Mwenyekiti
wa Kamati hiyo Mheshimiwa Timotheo Mnzava (Mb) ametoa pongezi hizo leo katika
siku yake ya kwanza ya ziara ya kikazi mkoani Tabora wakati ziara ya kukagua
miradi mbalimbali ya sekta ya misitu na nyuki huku akitaka juhudi hizo ziongeze
ili kukamilisha kabisa kazi zilizobaki kwa baadhi ya miradi.
Kamati
imefika jana ambapo inaendelea kesho kwa mkoa wa Tabora na Singida imeambatana
na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dustan Kitandula (Mb), Katibu
Mkuu, Dkt. Hassan Abbasi na baadhi ya Watendaji wa Wizara na taasisi zilizo
chini ya Wizara.
Mwakilishi
wa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Mheshimiwa Deusdedith Katwale pia
ameipongeza na kuishukuru Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuleta ubunifu
na wa kuanzisha nembo (trade mark)
maalum inayotambulisha asali kimataifa.
“Napenda
kuishukuru na kuipongeza Wizara ya Maliasili na utalii kwa mapinduzi makubwa
kwenye sekta hii kwa kuanzisha nembo ya asali yetu ambayo itasaidia
kuitambulisha asali ya Tanzania kwenye masoko ya kimataifa hivyo kuuza asali kwenye masoko ya
kimataifa tofauti na awali,” amefafanua Mhe. Katwale.
Katika
miradi hiyo Mfuko wa Misitu Tanzania umetoa ruzuku kwa miradi 56 katika Mkoa wa
Tabora pekee yenye thamani ya takribani shilingi bilioni 2.2.
Miradi hiyo
inatekelezwa katika Wilaya zote 7 za Mkoa wa Tabora ambazo ni Tabora, Uyui,
Nzega, Igunga, Sikonge, Urambo na Kaliua.
Aidha, kati
ya miradi hiyo ipo miradi ya ufugaji nyuki inayotekelezwa zaidi na vikundi vya
kijamii, viwanda vya mazao ya nyuki na miradi ya kuimarisha Chuo cha Mafunzo ya
Ufugaji nyuki Tabora (BTI).
Pia Mfuko
unagharamia ujenzi wa kiwanda na ununuzi wa mitambo kwa ajili mafunzo ya
kuchakata na kufungasha mazao ya nyuki katika Chuo cha BTI kwa ajili ya mafunzo
kwa vitendo kwa wanafunzi.
Kamati, pia imepata bahati ya kutembelea na kujionea mradi wa ukarabati wa jengo la utawala la Chuo, ujenzi wa jengo la karakana ya mbao kwa ajili ya kuwezesha utoaji wa mafunzo ya utengenezaji wa mizinga bora ya nyuki, ujenzi wa jengo la ukumbi wa mihadhara (lecture theatre) kwa matumizi wanafunzi wa BTI na Kituo cha ufugaji nyuki kibiashara kilianzishwa kama mkakati wa kuongeza kipato cha jamii kwa uboreshaji wa uchumi na kupunguza uharibifu wa misitu ya hifadhi katika Mkoa wa Tabora.
Na. John Mapepele- Tabora



0 Maoni