Imeelezwa
kwamba ujenzi na matengenezo ya barabara na madaraja unaofanywa na Wakala ya Barabara
za Vijijini na Mijini (TARURA) wilayani Babati unaenda kufungua shughuli za
utalii.
Mkuu wa
Wilaya ya Babati Mhe. Emmanuella Kaganda ameeleza hayo alipofanya mahojiano na
waandishi wa habari ofisini kwake wilayani humo, Mkoani Manyara hivi karibuni.
Mhe. Kaganda
amesema kufunguka kwa mtandao wa barabara kumeweza kuvutia watalii katika mbuga
za Taifa za Tarangire na Manyara, utalii wa kitamaduni, Ziwa Manyara pamoja na
milima ambayo wananchi hufanya shughuli za kitalii.
“Babati
inaenda kufunguka kwani mtandao wa barabara unaendelea kuongezeka kwa kuwa na
Kilomita 1,548.792 ambapo Mji wa Babati una Km. 595.102 na Halmashauri ya
Babati Km. 953.69,”alisema na kuendelea,
“Hakika kazi
kubwa inafanyika na Serikali ya Awamu ya Sita kwani Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu
Hassan ameendelea kutupatia pesa za kuwekeza kwenye miundombinu,” alisisitiza.
Ameongeza
kuwa katika mwaka wa fedha 2024/2025 TARURA wilaya ya Babati imepanga kutumia
zaidi ya shilingi bilioni 4.9 kwaajili ya kuchonga barabara, kutengeneza barabara
za changarawe, kujenga madaraja na Papu Kalavati.
Aidha,
amesema katika kipindi cha miaka mitatu wamepokea jumla ya shilingi bilioni 12
kwaajili ya kuimarisha mtandao wa barabara ambapo awali TARURA walikuwa
wakipokea bilioni 1 hivyo ongezeko la bilioni 3.5 ni ongezeko kubwa katika
wilaya hiyo.
“Ongezeko
hili sio kidogo na tumeona namna Mhe. Rais alivyoamua kuibadilisha Babati
yetu,” aliongeza kusema.
Hata hivyo
Mhe. Kaganda alisema katika matengenezo hayo wanatarajia kufunga taa zipatazo
90 katika barabara ya kuelekea hospitali ya wilaya ya Mrara ili kulinda usalama
wa wananchi wakati wakielekea kupata huduma nyakati za usiku.
Hivyo ametoa
rai kwa wananchi wa wilaya hiyo kuitunza miundombinu inayojengwa na Serikali na
kuepuka kufanya shughuli za kilimo kandokando ya barabara na kupitisha majembe
yanayokokotwa na wanyama ili kuepuka mmomonyoko wa ardhi.
Pia
aliwataka wananchi kusafisha mitaro iliyopo mbele za nyumba zao, kutokutupa
taka hovyo na hivyo kutunza mitaro ya maji hususani kipindi hiki cha mvua ili
kuepuka mafuriko na magonjwa mbalimbali yanayotokana na uchafu.
Naye, Bw.
Hamis Rajabu Mkazi wa Mtaa wa Mrara amesema madaraja waliyojengewa katika
barabara hiyo ambayo ni kiunganishi kati ya Babati Mjini na Vijijini yameweza
kuwaondolea kero mbalimbali zilizokuwa zikiwakabili hususan kipindi cha masika
ambapo magari na vyombo vingine vya moto vilikuwa vikipita kwa kupokezekana.

0 Maoni