CHAMA Cha
Mapinduzi (CCM) kimeiomba Wizara ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali
za Mitaa (TAMISEMI), kuwaelekeza wasimamizi Uchaguzi wa Serikali za Mitaa,
kupuuza makosa madogo madogo yaliyotokea, ili kuruhusu wagombea wengi kushiriki
uchaguzi huo.
Akizungumza
na wahariri na waandishi waandamizi wa vyombo vya hahari nchini, Katibu Mkuu wa
CCM, Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, ametoa mfano wa makosa hayo
yanayostahili kupuuzwa ni pamoja na wagombea kukosea herufi.
Kupitia
mkutano huo uliofanyika Ofisi Ndogo za Makao Makuu ya CCM, Lumumba, jijini Dar
es Salaam, leo Novemba 12, 2024, Balozi Nchimbi amesema ni vyema TAMISEMI
ikaangalia uwezekano wa kuwarudisha wagombea wote walioenguliwa kutokana na
makosa hayo madogo madogo ili kuhamasisha ukuaji wa demokrasia kwenye uchaguzi
huo.
Aidha,
kuhusu sehemu kubwa ya malalamiko mengi ya kuenguliwa kuonekana ni ya wagombea
wa vyama vya upinzani, Balozi Nchimbi amewatoa shaka Watanzania kuwa, si kweli
kwamba wagombea walioenguliwa ni wale wa vyama vya upinzani pekee, bali pia
hata wagombea wa CCM wapo waliowekewa mapingamizi ya kugombea.
“Waziri wa
TAMISEMI tunajua anafuata sheria, lakini ni muhimu kutambua demokrasia yetu hii
bado ni changa hivyo tunahitaji muda wa kuendelea kujiÃfunza…tunaziomba mamlaka
hasa TAMISEMI katika nyakati za mwisho za rufaa kuyapuuza makosa madogo madogo
ili watu wengi wapate nafasi ya kugombea," alisema Dkt. Nchimbi.


0 Maoni