Katika muendelezo wa juhudi za kukabiliana na majanga ya moto wa msituni leo tarehe 18 Oktoba 2024 Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania kupita Shamba la Miti Saohill kwa kushirikiana na ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mufindi wamefanya kikao na madiwani, watendaji wa kata pamoja na maafisa tarafa wa wilaya ya Mufindi ili kujadili juu ya namna kuendelea kukabiliana na matukio ya moto misituni.
Akuzungumza wakati wa Kikao hicho,
Katibu Tawala wa Wilaya ya Mufindi Ndg. Mashaka Mfaume amesema kuwa uchumi wa
Wilaya ya Mufindi unategemea uwepo wa misitu na biashara ya mazao ya misitu
hususani kutoka katika Shamba la Miti Saohill hivyo ni muhimu kuhakikisha kuwa
kunakuwa na mikakati ya pamoja ya pande zote kuhakikisha rasilimali za misitu
zinatunzwa.
Katika kikao hicho pia aliwakumbusha
viongozi wa vijiji wote (Madiwani, Watendaji na Maafisa Tarafa) majukumu yao
katika kuhakikisha misitu haithiriwi na moto ikiwa ni pamoja na kusimamia
utekelezaji wa sheria na taratibu ndogo ndogo za halmashauri pamoja na zile za
vijiji zinahusu matumizi sahihi ya moto zinatekelezwa kwa usahihi na wananchi
katika vijiji vyao.
Sambamba na hayo ameelekeza mambo
mbalimbali ambayo kiongozi katika eneo husika anaweza kuyafanya ili kudhibiti
majanga ya moto ikiwa ni pamoja na utoaji wa elimu na uhamasishaji juu ya
madhara ya moto, kushirikiana na wataalam wa misitu, kujenga vikundi vya
kujitolea, kufuatilia utekelezaji wa sheria na taratibu za matumizi ya sahihi
ya moto pamoja na kuunda timu au kamati za viongozi wa kudhibiti matukio ya
moto.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa
Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi Ndg. Festo Elia Mgina amesema kuwa viongozi
katika ngazi za kata na vijiji kuwajibika na kuwa mfano wa kwanza katika
utekelezaji wa sheria na taratibu zilizowekwa kuhusu ulinzi wa misitu dhidi ya
matukio ya moto kichaa ambayo yamekuwa yakileta hasara kubwa kwa serikali na
wananchi katika Wilaya ya Mufindi.
Aidha amewataka madiwani na watendaji
wote kuhakikisha sheria na taratibu zilizowekwa zinaendelea kusomwa na
kukumbushwa mara kwa mara kwa wananchi katika mikutano ya vijiji ili
kuhakikisha madhara yatokanayo na moto yanadhibitiwa na kuepuka athari zinazojitokeza.
0 Maoni