Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imeendelea kuboresha huduma za usafiri na usafirishaji kwa kujenga barabara, vivuko na madaraja katika maeneo mbalimbali mkoani Katavi ili kuinua shughuli za kijamii na kiuchumi.
Akizungumza na waandishi wa habari
Kaimu Meneja wa TARURA Mkoa wa Katavi, Mhandisi Japhet Bengesi alisema,
Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya kazi kubwa katika kuimarisha
miundombinu ya barabara mkoani Katavi.
Mhandisi Japhet amemshukuru Rais Samia
kwa kuongeza bajeti ya TARURA mkoa wa Katavi kutoka Shilingi Bilioni 4 hadi
kufikia Shilingi Bilioni 15 ambayo kwa kiasi kikubwa imesaidia kuimarisha
mtandao wa barabara mkoani humo.
"Tumeweza kufungua barabara mpya ambazo
hazikuwepo kabisa zenye urefu wa Km 439, barabara za changarawe zimeongezeka
kutoka Km 471 hadi Km 692 ambalo ni ongezeko la Km 221 na barabara za lami
kutoka Km 36 mpaka Km 53 ambalo ni ongezeko la Km 17 ndani ya miaka mitatu
ambapo ni mafanikio makubwa," alibainisha.
“Barabara za lami zimejengwa katika
maeneo ya mijini na katika huduma za kijamii kama vile hospitali za wilaya
ambapo katika wilaya ya Tanganyika tumejenga Km 1 ya lami ambayo imegharimu
shilingi milioni 500,” alisema.
Aidha, alisema kuwa wameendelea
kutumia teknolojia mbadala ya ujenzi wa madaraja ya mawe ambayo ni gharama
nafuu kulinganisha na madaraja ya zege ili kuwaunganisha wananchi katika maeneo
ya vijijini katika shughuli zao za biashara na huduma za kijamii na kiutawala.
Alisema wamejenga madaraja 19 ya mawe
likiwemo daraja la mto Mwali pamoja na barabara zake ambalo limegharimu
shilingi milioni 283 ujenzi wa madaraja haya yamekuwa ni mkombozi mkubwa sana
kwa wananchi kwani wanafikia huduma za kijamii kwa urahisi.
Vilevile, alieleza kuwa TARURA mkoa wa
Katavi imetekeleza miradi ya kimkakati inayogusa wananchi moja kwa moja, katika
Halmashauri ya Mpimbwe Wilaya ya Mlele wamejenga daraja la mto Msadya lenye
urefu wa mita 60 kwa gharama ya shilingi Bilioni 4.2 ili kurejesha mawasiliano
ya wananchi wa kata za Mwamapuli, Chamalendi, Ikuba, Kibaoni na Majimoto.
Naye, Mwenyekiti wa kijiji cha
Mwamapuli B wilayani Mpimbwe, Bw. Zengo Fareji, ameishukuru serikali kwa
kujenga la Msadya ambalo limewasaidia kusafirisha mazao yao sokoni kwa urahisi.
Kwa upande wake, Bw. Nkolingo Selemani
mkazi wa kijiji cha Majalila wilayani Tanganyika, ameishukuru serikali kwa
ujenzi wa daraja la mto Mwali ambalo linaunganisha vijiji vya Nyagantambo,
Ifinsi na Bugwe kwani limewasaidia kusafirisha mazao yao na kuzifikia huduma za
kijamii kiurahisi.
0 Maoni