WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema suala la uhifadhi wa
mazingira liwe ajenda ya Kitaifa na jukumu la kila mmoja kuanzia ngazi ya
familia mpaka Taifa.
“Na tunapokwenda kuhifadhi mazingira lazima tuanze na ngazi
ya familia na tunapopanda juu tupanue wigo hadi kwa wadau mbalimbali. Viongozi
wa dini mnayo nafasi kubwa na hii lazima iwe ajenda maalum, iwe ni ofisi za
umma, za binafsi au kwenye taasisi.”
Ametoa kauli hiyo leo (Jumanne, Septemba 10, 2024) wakati
akifunga mkutano maalum wa viongozi na wadau wa mazingira ulioitishwa ili
kujadili mwenendo wa mazingira nchini. Mkutano huo ulifanyika kwenye Kituo cha
Mikutano cha Jakaya Kikwete, jijini Dodoma.
Amesema kitendo hicho
kitakuwa ni kuunga mkono juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuendelea
kuimarisha uhifadhi na Usimamizi wa mazingira nchini, kazi aliyoifanya kwa
weledi, ustadi na mafanikio tangu akiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania.
“Amemudu kusimamia na kutoa miongozo mahsusi ya kuhakikisha
mazingira yanahifadhiwa. Leo hii, yeye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na tunamuona anaendelea kulisimamia ili Taifa lifanikiwe katika
uhifadhi wa mazingira kwa vizazi vya sasa na baadaye,” amesema.
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwaeleza wajumbe wa mkutano
huo juu ya jitihada ambazo Rais Dkt. Samia amekuwa akizichukua ili kuhakikisha
suala la nishati safi linakubalika.
"Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuja na
dhana mpya ya kukataa kukata miti na kutuhamasisha kuhusu nishati safi ya
kupikia. Rais wetu amekuwa kinara wa nishati safi hadi na mwezi Mei alienda
Ufaransa kuhutubia kuhusu nishati safi na yeye akiwa ni Mwenyekiti mwenza wa
mkutano huo. Hii ni fahari kwa nchi yetu," amesema.
Amesema Serikali imetoa fursa kwa wajasiriamali kuanzisha
biashara ya kuuza mitungi na majiko ya gesi hadi kwenye ngazi ya vijiji ili
nishati hiyo iweze kupatikana kwa urahisi. “Huko mbele tutaweka ukomo wa
matumizi ya mkaa na kuni,” ameongeza.
Katika kukabiliana na changamoto za uchafuzi wa mazingira,
Waziri Mkuu amesema Serikali imechukua hatua za kisera na kimkakati ili kuleta
matokeo chanya. Amezitaja hatua hizo
kuwa ni kuandaliwa kwa Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 2021; Kutungwa kwa
Sheria ya Mazingira ya mwaka 2014; kuandaa na kutekeleza Mpango Kabambe wa
Taifa wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira wa mwaka 2022 hadi 2032; kuandaa na
kutekeleza Mkakati wa Kitaifa wa kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi wa
mwaka 2021 hadi 2026; na kutungwa kwa Kanuni na Miongozo inayohusu masuala ya
Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu ameitaka wizara inayosimamia
mazingira ishirikiane kwa karibu na wizara za kisekta kuhakikisha maadhimisho
mbalimbali ya Kitaifa yanayogusa masuala ya mazingira yanatumika kikamilifu
kuwezesha jamii kupata uelewa na kuweka alama za kudumu na matokeo yanayopimika
kuhusu utunzaji mazingira ikiwemo Siku ya Upandaji Miti, Siku ya Hali ya Hewa,
Siku ya Maji, Siku ya ardhi Oevu, Siku ya Mazingira na Siku ya Hifadhi ya
Tabaka la Ozoni.
Kuhusu kuimarisha utoaji wa elimu na uhamasishaji kuhusu
utunzaji wa mazingira, Waziri Mkuu amezitaka Ofisi za Mikoa na Wilaya zisimamie
suala hilo na kusisitiza kuhusu umuhimu wa kuzingatia sheria na kanuni za
mazingira na ikibidi watumie mitandao ya kijamii kusambaza elimu hiyo.
"Kuongezeka kwa ufahamu miongoni mwa jamii kuhusu
umuhimu wa uhifadhi wa mazingira kutasaidia kupunguza uharibifu na kuimarisha
usimamizi wa mazingira. Aidha, elimu ijumuishe matumizi endelevu ya rasilimali
za mazingira ikiwemo matumizi bora ya ardhi, maji, na nishati ili kuhakikisha
kuwa rasilimali hizi zinabaki kuwa za kudumu kwa vizazi vijavyo,"
amesisitiza.
Mapema, Waziri wa Nchi (OMR - Muungano na Mazingira), Dkt.
Ashatu Kijaji alisema mkutano huo maalum ulihudhuriwa na washiriki 2,500 kutoka
maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Zanzibar. "Ninauita huu ni mkutano mkuu
maalum kwa sababu umehusisha makundi tofauti ya kijamii wakiwemo viongozi wa
dini, wa kisiasa, wa kimila, wanafunzi, wabunge na wadau wengine."
Alisema ofisi yake itafuatulia ukamilishajinwa rasimu ya
Azimio la Dodoma hadi liwe Azimio kamili kwani linahitaji kufuata utaratibu wa
Serikali hadi lije kuzinduliwa rasmi.
Azimio la Dodoma liliwasilishwa mbele ya wajumbe wa mkutano
huo na Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu, Balozi Dkt. Bashiru Kakuru. Baadhi ya
maeneo yaliyotajwa ni usimamizi na mapitio ya sera na sheria hasa za misitu na
uhifadhi; uwajibikaji na ushirikishwaji wa umma kupitia ugatuzi wa madaraka;
usimamizi wa taka ngumu na usafi wa mazingira; upandaji wa miti, mabadiliko ya
tabianchi na biashara ya kaboni; utoaji wa elimu kuhusu nishati safi; uchumi wa
bluu, rasilmali fedha na elimu kwa umma kuhusu mazingira.
CHANZO: Ofisi ya Waziri Mkuu
0 Maoni