Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila inaendelea na kambi
maalum ya upasuaji wa upandikizaji wa meno bandia kwa njia ya kisasa ambayo
inafanyika kwa muda wa siku tano kuanzia Septemba 10 hadi 14, 2024.
Kambi hiyo inayofanywa na wataalam wa ndani kwa kushirikiana
na Daktari Bingwa aliyebobea katika upasuaji wa taya kutoka Hospitali za
Wochhardt Dkt. Chirag Desai ambapo kwa kipindiki hiki cha siku tano wanatarajia
kufanya upandikizaji kwa wagonjwa 30.
Upandikizaji huu wa meno bandia utahusisha kupandikiza jino
la mgonjwa moja kwa moja kwenye mfupa wa taya yake na kulifanya jino hilo
kujishikiza moja kwa moja kama jino la kawaida hivyo haliwezi kutoka kama
yalivyo meno mengine ya bandia.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Idara ya Kinywa na Meno, Dkt. Agrey
Shao mwitiko wa watu kufanya upasuaji wa kupandikiza meno bandia umekuwa mkubwa
ambapo hapo awali walilenga kupandikiza wagonjwa 20 na hivyo idadi ya
wanaopandikizwa imezidi malengo waliojiwekea kulingana na mahitaji ya walio
wengi.
Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila imeendelea kufanya matibabu ya ubingwa bobezi ambayo yamesaidia kupunguza rufaa na usumbufu wa Watanzania kwenda nje ya nchi kutafuta matibabu hayo ambayo yanagharimu kiasi kikubwa cha fedha.
0 Maoni