TFS na Zimamoto wauzima moto katika Milima ya Uluguru

 

Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa kushirikiana na Jeshi la zimamoto mkoa wa Morogoro wamefanikiwa kuzima moto uliozuka katika milima ya Uluguru iliyopo katika msitu wa Hifadhi wa Mazingira Asilia Uluguru.

Akizungumza kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Prof.  Dos Santosi Silayo, Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Msitu wa Mazingira Asilia Uluguru, PCO. Bernadetha Chile amesema; wamefanikiwa kwa asilimia mia moja kudhibiti moto huo uliozuka kuanzia Septemba 14, 2024.

Amesema moto ulianzia kuwaka nje ya Hifadhi eneo la Bigwa Kisiwani Kata ya Bigwa Manispaa ya Morogoro kwa wakulima wanaoandaa mashamba kwaajili ya msimu mpya wa Kilimo na baadae ukafika katika Hifadhi ya Milima ya Uluguru. Moto huo ulisambaa eneo kubwa la msitu hadi upande wa pili wa msitu katika eneo la Nughutu, moto huo ulidhibitiwa. Mnamo tena Septemba 15 , 2024 moto uliibuka maeneo ya Ualimu na kufanikiwa kuudhibiti.

Pia jana Septemba 16,2024  moto mwingine uliibuka eneo la Bong’ola na eneo la ofisi za UNFR na kufika juu zaidi ambapo umedhibitiwa kwa kuzima visiki na pia zimewekwa Fire break ili kuhakikisha hakuna madhara tena ya moto katika maeneo hayo.

Pamoja na kufanikiwa kuuzima moto katika maeneo yote ulikojitokeza bado ufuatiliaji wa karibu unaendelea katika maeneo hayo yote na mengine ili kubaini kama kuna dalili zozote za moto na kuzishughulikia haraka kabla hazijaleta madhara tena,” amesema Mhifadhi Chile.

Pia Mhifadhi ametoa wito kwa watu wote wanaoishi karibu na hifadhi ya msitu wa mazingira asilia ya Uluguru kuwa mstari wa mbele katika kulinda na kuhifadhi msitu huo kwani ndio uti wa mgongo wa mito inayotegemewa kuzalisha maji na kusambazwa katika mikoa ya Pwani, Dar es Salaam na Morogoro yenyewe.



Chapisha Maoni

0 Maoni