Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi
Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amesema Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa
na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imedhamiria kuwafanya wananchi kuwa kitovu
cha maendeleo kwa kuhakikisha wanakuwa na fikra chanya katika maendeleo, yenye
maadili mema, malezi na makuzi chanya ya watoto, jamii isiyo na ukatili wa
kijinsia, yenye uzalendo kwa nchi yao.
Waziri Dkt. Gwajima ameyasema hayo jana Septemba 16, 2024
wilayani Tarime mkoani Mara wakati wa ziara ya kuhamasisha jamii kupambana na
vitendo vya ukatili.
Waziri Dkt. Gwajima amesema lengo la Wizara yake ni
kuhakikisha jamii inaelimika kimaendeleo kwa inayofanya kazi kwa bidii na
kujitoa, kujali na kuhifadhi rasilimali za nchi, kuwa na lishe na afya bora,
matumizi sahihi ya TEHAMA, jamii inayojiwekea akiba, jamii yenye uwezo wa
kuzitambua na kuzitatua changamoto zao kwa kushirikiana na Serikali.
Ameeleza jamii isiyo na ukatili inakuwa na mazingira mazuri
ya kufanya shughuli za maendeleo hivyo Serikali itaendelea kushirikiana na
wadau mbalimbali kutoa elimu na fursa ili jamii iweze kujiwamua kiuchumi na
kupambana na vitendo vya ukatili.
"Natoa rai kwa viongozi, wataalamu wa Maendeleo ya
jamii na Ustawi wa jamii kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo kujenga mazingira
rafiki ili kuwasaidia wananchi kufanya shughuli za maendeleo bila hofu wala woga
dhidi ya vitendo vya ukatili," amesema Waziri Dkt. Gwajima.
Amesema katika kuhakikisha jamii inakuwa na ustawi, Serikali
kwa kushirikiana na wadau inatekeleza afua zinazolenga kumaliza changamoto
zinazosababisha ukatili zikiwemo kuimarisha uchumi wa kaya kwa kuendelea kutoa
mikopo yenye masharti nafuu, kutoa elimu kuhusiana na mila na desturi zenye
madhara na kuimarisha mila zenye matokeo chanya.
Amezitaja afua nyingine kuwa ni kuimarisha ulinzi wa
mwanamke na mtoto katika maeneo ya umma na katika mitandao, kuongeza vituo vya
kutolea huduma kwa wahanga wa ukatili kama vile nyumba salama na vituo vya
mkono kwa mkono na kwa kiwango kikubwa kushirikisha wanaume katika kutokomeza
vitendo vya ukatili.
Ameupongeza mkoa wa Mara kwa ujumla kwa jitihada za
kutokomeza ukatili wa kijinisa ambapo kwa mujibu wa utafiti wa Afya ya Uzazi na
Mtoto na Viashiria vya Malaria Tanzania (TDHS) kwa mwaka 2015/2016, ukeketaji
umepungua kutoka asilimia 32 (2016) hadi 28 (2022), huku vitendo hivyo
vikiongoza katika mikoa ya Arusha (43%) na Manyara (43%).
Aidha, Waziri Dkt. Gwajima amewapongeza wananchi wa Kata ya
Ganganye kwa kuonesha uzalendo katika masuala ya kimaendeleo na kutatua
changamoto mbalimbali ikiwemo ukatili wa kijinsia, amesema jamii ndio sehemu
pekee katika kuhakikisha wanaondokana na vitendo vya ukatili.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Tarime Meja Edward Gohele amesema
wataendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kufikisha elimu ya
kupambana na vitendo vya ukatili ili jamii iondokane na vitendo hivyo na
kujikita katika shughuli za maendeleo katika maeneo yao.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Kivulini Yassin Ali
amesema Shirika hilo linashirikiana na Serikali katika kuhakikisha inafikia
Jamii kutoa elimu na kuhamasisha kupambana na vitendo vya ukatili katika maeneo
yao.
"Mhe. Waziri katika kupambana na vitendo vya ukatili sisi Shirika la Kivulini tumekuja na mbinu za kutumia ushabiki wa Mpira kwa timu za Simba na Yanga ili kuishirikisha Jamii katika kupambana na vitendo vya ukatili," amesema Ali.
Na. WMJJWM- Tarime Mara
0 Maoni