Maporomoko ya Sanje yawastaajabisha Madiwani Masasi

 

Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Hifadhi ya Taifa Milima Udzungwa, Theodora Aloyce, amesema wananchi wanaoishi kando ya Hifadhi ya Milima Udzungwa wamekuwa wanufaikaji wakubwa kiuchumi kutokana na kufanya biashara ya utalii kwa kuuza mazao ya utalii ambayo yamekuwa kivutio kikubwa kwa wageni wanaotoka nje, ikiwemo utalii wa vyakula vya asili na matunda kama madafu, ambayo yameongeza thamani ya Hifadhi hiyo.

Kamishna Msaidizi Aloyce ameyasema hayo jana wakati akiwapokea wageni kutoka Halmashauri ya Mji wa Masasi, wakiwemo Madiwani pamoja na wakuu wa idara, waliotembelea Hifadhi ya Milima Udzungwa, lengo likiwa ni kujionea upekee wa Hifadhi  hiyo yenye maporomoko ya maji ya mita 170, spishi za mimea, wanyamapori wa kipekee, na ndege wa ajabu.

“Katika vijiji vyetu tumeweka mahusiano mazuri baina yetu sisi wahifadhi pamoja na wananchi wakazi wa hapa. Wamejifunza namna ya kuongeza thamani ya utalii wa vyakula vya asili, wamekuwa wanauza vikapu, bangili pamoja na madafu ambapo wageni wengi, hususan watalii kutoka nje, wanafurahia madafu ya Udzungwa kutokana na historia ya matunda hayo,” alisema Afande Aloyce.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Masasi, Mhe. Hashimu Namtumba, alisema lengo la wao kutembelea Hifadhi hiyo ni kuunga mkono jitihada za Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuutangaza utalii wa maliasili za Taifa pamoja na kuwa mabalozi wazuri katika kuhifadhi na kutunza rasilimali za nchi.

“Kwakweli ni Hifadhi nzuri sana. Tumefurahia kujionea maporomoko ya maji. Mengi tumekuwa tukisikia tu, lakini leo tumepata historia na kujua baadhi ya wanyama, ikiwemo nyani wa Ngolanga wanaopatikana hapa tu katika ulimwengu wote, pamoja na ndege wengi wa kipekee,” alisema Mhe. Namtumba.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Masasi, Bi. Remada Mbowe, alielezea namna upekee wa Hifadhi  ya safu ya Milima Udzungwa utakavyoenda kuimarisha mawazo yao katika utendaji wa shughuli zao za kila siku, kwani mazingira yake yanaburudisha na yanapunguza msongo wa mawazo kwa mtu yeyote atakayefika katika mandhari ya Hifadhi  hiyo.

“Kwakweli katika Hifadhi  hii tumeona vitu vizuri. Mimi binafsi nilipofika katika haya maporomoko ya maji nilishindwa kujizuia, nilikimbilia haya maji, kwakweli ni mazuri sana. Watanzania sasa waone haja ya kutembelea Hifadhi hii kwani nimejionea mengi na mengine yanajenga akili zetu upya,” alisema Bi. Remada.

Hifadhi ya Taifa ya Milima Udzungwa inatambulika kama Hifadhi pekee yenye uzuri unaovutia bionuai kubwa. Maporomoko yake ya maji yenye mita 170 yanaifanya Hifadhi hiyo kuwa na umuhimu mkubwa katika uhifadhi wa maji ambayo ni chanzo muhimu cha mito inayohudumia katika maeneo ya karibu.

  Na: Zainab Ally-Udzungwa

Chapisha Maoni

0 Maoni