Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko
jana Septemba 6, 2024 jijini Dodoma amekutana na kufanya mazungumzo na balozi
mpya wa Uingereza nchini. Mhe. Marianne Young.
Lengo la mazungumzo hayo likiwa ni kujitambulisha kwa balozi
huyo pamoja na kujadili masuala ya kipaumbele ya ushirikiano baina ya Tanzania
na Uingereza katika sekta ya nishati.
Aidha, katika mazungumzo hayo, Dkt.Biteko amepongeza
ushirikiano mzuri uliopo baina ya Tanzania na Uingereza katika sekta mbalimbali
hususan sekta ya nishati kupitia ufadhili wa fedha kiasi cha shilingi bilioni
11.16 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo Songas kupitia
taasisi zake za mitaji za Shirika la UK Export Finance (UKEF) na Shirika la
Uwekezaji la Uingereza (BII).
‘‘Serikali itaendelea
kushirikiana nanyi katika sekta ya nishati
sambamba na kuikaribisha sekta binafsi kutoka nchini Uingereza kuja kuwekeza Tanzania katika uzalishaji, uhifadhi na usambazaji wa
nishati hususan nishati safi ya kupikia na nishati mbadala, ’’ amesema Dkt.
Biteko.
Kwa upande wake, Balozi Young, ameipongeza Tanzania kwa
uongozi wake katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia barani
Afrika na kusema kuwa nchi yake itaendelea kuunga mkono sekta ya nishati
nchini.
Mazungumzo hayo yamehudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki Mhe. Denis Londo.
0 Maoni