Washikiliwa na Polisi Mbeya kwa kukutwa na silaha

 

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia Sebastian Thomas [37] Dereva, Mkazi wa Isanga Jijini Mbeya na Silvester Mashaka Mashauri [40] Mkazi wa Iganzo Jijini Mbeya kwa tuhuma za kupatikana na silaha bunduki aina ya Shotgun yenye namba za usajili C328809 bila kuwa na kibali cha umiliki wa silaha hiyo.

Mtuhumiwa Sebastian Thomas [37] alikamatwa akiwa na silaha hiyo akiwa ameificha kwenye mfuko wa sandarusi na kuiweka nyuma ya kiti cha Dereva ndani ya Gari namba T.844 DME Tata inayosafirisha abiria kati ya Mbeya kwenda Chunya.

Taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya SACP Benjamin Kuzaga imesema mtuhumiwa baada ya kukamatwa alieleza kupewa silaha hiyo na mtuhumiwa Silvester Mashaka Mashauri kwa ajili ya kwenda kutumika katika shughuli za ulinzi machimboni katika kampuni binafsi.

Sambamba na hilo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia Lugano Tutufye [29] Mkazi wa RRM Ilomba Jijini Mbeya kwa tuhuma ya kupatikana na silaha ya wizi Bastola aina ya Browing ikiwa na risasi zake 9 ndani ya magazine mali ya Said Mussa Mwatuka [46] Mkazi wa Chamanzi Dar es Salaam.

Awali Agosti 04, 2024 eneo la PM Hotel lililopo Nanenane Jijini Mbeya Said Mussa Mwatuka [46] aliibiwa Silaha Bastola iliyokuwa ndani ya Gari lake aina ya Subaru Impleza rangi nyekundu yenye namba za usajili T.410 DYB baada ya mtuhumiwa ambaye alimpakiza kama abiria kuiba silaha hiyo na kuondoka nayo.

Ufuatiliaji ulifanyika na Agosti 05, 2024 huko maeneo ya Nanenane Jijini Mbeya mtuhumiwa alikamatwa akiwa na silaha hiyo na risasi zake ndani ya magazine. Mtuhumiwa anaendelea kuhojiwa na atafikishwa mahakamani.

Aidha, katika kukabiliana na uingizaji wa bidhaa za magendo nchini, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watuhumiwa watano kwa tuhuma za kuingiza nchini sukari kwa njia ya magendo. Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Maafisa wa bodi ya sukari nchini liliendesha oparesheni ya pamoja Julai 25, 2024 na kukamata kiasi cha kilogramu 420 za sukari zilizoingizwa nchini bila kibali kutoka nchini jirani ya Malawi na Zambia.

Watuhumiwa waliokamatwa katika oparesheni hiyo ni  Oria Mwakaselema [48] Mkazi wa Mwakibete, Anyosisye Mwambona [63] Mkazi wa Ilomba, Fredy Nyangalima [57] Mkazi wa Uwanja wa Ndege wa Zamani, Itika Mwanyula [28] Mkazi wa Forest na Jenny Seme [52] Mkazi wa Isyesye Jijini Mbeya.

Chapisha Maoni

0 Maoni