Utalii wa michezo wazidi kuitangaza Hifadhi ya Taifa Mikumi

 

Ukiondoa Maveterani wa SIMBA na YANGA kushindana katika uwanja wa mpira wa miguu uliopo ndani ya Hifadhi ya Taifa Mikumi na kufuatiwa na Uzinduzi wa Jezi mpya ya SIMBA SPORT CLUB “UBAYA UBWELA”,  jana iliandikwa historia nyingine kwa timu ya mpira wa miguu kutoka PENSACOLA CHRISTIAN COLLEGE ya nchini Marekani kusakata kabumbu ndani ya hifadhi pamoja na kufanya utalii.

Mchungaji, Jerry M Wyatt wa kanisa la Faith Baptist lililoko Morogoro ambae pia ni mwenyeji wa kundi la watalii hao kutoka Marekani alisema kuwa wamefurahishwa sana kutembelea hifadhi hiyo na kupata wasaa wa kucheza mechi ya kirafiki ndani ya hifadhi hiyo.

Vilevile, amewasisitiza watanzania kutembelea Hifadhi ya Taifa Mikumi na kujionea uumbaji wa Mungu kwani ipo karibu sana na Mkoa wa Morogoro, Pwani na Dar es Salaam.

Naye, Afisa Mwandamizi wa Uhifadhi Herman Baltazari alisema hifadhi hiyo imeanza kusheherekea maadhimisho ya miaka 60 tangu kuanzishwa kwake tarehe 7 Agosti 1964.

Mwifadhi Herman alisema, “Katika kuadhimisha miaka 60 tumeanza kwa kukata keki tukiwa pamoja na hili kundi la wageni kama ishara ya kuendelea kuhifadhi eneo hili lililojaliwa kuwa na maliasili nyingi kwa faida ya kizazi cha sasa na baadae.”

Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Fredrick Malisa alisema kuwa mechi hii ya kimataifa inaendelea kukuza zao jipya la utalii wa michezo ndani ya hifadhi ya taifa Mikumi na alitumia fursa hiyo kuwakaribisha taasisi na watu binafsi kuja kusheherekea Mabonanza, Family Days pamoja na michezo mbalimbali ndani ya hifadhi.

Malisa aliongeza, “Serikali imeendelea kuboresha na kuongeza miundombinu mbalimbali ya utalii wa michezo na sasa mechi za mpira wa mikono na mpira wa kikapu zinaweza kuchezwa ndani ya hifadhi hii.”

TANAPA imeendelea kuboresha miundombinu mbalimbali ndani ya Hifadhi za Taifa ili kuendelea kuvutia watalii wengi zaidi na kuendelea kuvumbua mazao mbalimbali ya utalii ili kuwawezesha watalii kukaa muda mrefu hifadhini.


Na. Mwandishi wetu- Mikumi

Chapisha Maoni

0 Maoni